NPS: Ushindi wa kesi usishuke asilimia 85

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Sylvester Mwakitalu, amewataka waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwenda kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu huku wakilenga kufanikisha lengo la ushindi wa kesi mahakamani usiopungua asilimia 85.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakati wa kufunga mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa ofisi hiyo yaliyofanyika Julai 1 hadi 4, 2025 mjini Iringa, Mwakitalu amesema kuwa nafasi waliyoipata ni ya heshima na yenye jukumu kubwa la kulinda amani na usalama wa nchi kupitia usimamizi wa haki.

“Tunataka kila kesi mliyoisimamia, kama hamkuweza kushinda basi tulete sababu dhahiri kwanini imepotea. Hatujapata watu wa kuwaangalia wengine tu, bali wa kuhakikisha haki inatendeka. Ninyi ndio msingi wa mafanikio ya ofisi hii,” alisema Mwakitalu.

Ameongeza kuwa baadhi ya mikoa na wilaya tayari zimefanikiwa kufikia kiwango hicho cha ushindi wa kesi na kueleza kufurahishwa kwake kuona maeneo mengine kesi inasajiliwa na kuhitimishwa ndani ya wiki tatu tu kwa mafanikio makubwa.

Aidha, amewakumbusha waajiriwa hao kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni nyeti na inahitaji watumishi waadilifu, wachapakazi na wenye kujituma wakati wote na mahali popote.

Amesema ofisi hiyo iko katika hatua za kufungua ofisi zake katika kila wilaya hivyo hakuna mtumishi anayepaswa kuchagua eneo la kufanyia kazi.

“Ninyi mmebahatika kuchaguliwa kati ya wengi wenye sifa, itumieni nafasi hii kwa bidii na maarifa yenu yote,” alisema.

Akikazia majukumu ya kada mbalimbali, Mkurugenzi Mwakitalu aliwataka Makatibu Sheria kuzingatia ukusanyaji na usimamizi wa takwimu sahihi, na Madereva wa NPS kuendesha magari kwa uangalifu na kufuata sheria za barabarani, akisisitiza kuwa watakaofanya makosa watachukuliwa hatua kali ikiwemo kushtakiwa kama raia wengine.

“Ofisi hii ni ya haki, na haki lazima ionekane imetendeka. Tunawategemea sana, na kazi nzuri mtakayofanya itawafungulia milango ya mafanikio popote mlipo,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bibiana Kileo, amewataka waajiriwa hao kuiheshimu na kuiwakilisha vyema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia miiko ya kitaaluma.

“Hakuna sababu ya kutofanya kazi kwa weledi, huku mkizingatia kwamba mazingira na maslahi yameboreshwa tofauti na miaka minne iliyopita,” alisema.
Ameonya pia kuhusu mahusiano yasiyo na tija mahali pa kazi akisema, “Tusiendekeze mahusiano yasiyo na maana kazini.”

Naye Wakili wa Serikali kutoka mkoa wa Mtwara, Thimotheus Sullusi, aliyetoa shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, ameahidi kutekeleza yote waliyojifunza kwa bidii na uzalendo mkubwa kwa taasisi hiyo na Taifa.

Kwa upande mwingine, waajiriwa hao wapya walielezwa kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeweka mazingira mazuri ya kuwajali watumishi wake kupitia huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na uwepo wa Mfuko wa Rambirambi, unaosaidia watumishi katika nyakati za matatizo, pamoja na Mashtaka SACCOS—ambayo kwa sasa ina wanachama zaidi ya 900 nchini kote.

SACCOS hiyo imefanikiwa kujijengea mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 1.4, ambao unatumika kuwakopesha wanachama wake kwa ajili ya kutekeleza shughuli na majukumu mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Aidha, takribani Sh milioni 800 bado zipo kwenye mfuko wa SACCOS hiyo, mahsusi kwa ajili ya mikopo, na kinachosubiriwa ni wanachama kujitokeza ili kunufaika nazo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button