Prof Mkumbo aunga mkono juhudi za THRDC

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amepongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kuanzisha Mradi wa Ruzuku kwa Ajili ya Haki za Binadamu, ambao utasaidia kuongeza upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya shughuli za kulinda na kutetea haki za binadamu nchini.

Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mpango huo, ambapo pia amechangia Sh milioni moja kwaajili ya kuunga mkono utekelezaji wake.

Amesema kuanzishwa kwa mpango huo kunaonesha ubunifu na dhamira ya THRDC katika kutafuta vyanzo endelevu vya fedha vitakavyowezesha asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Hatua hii ni muhimu katika kujenga mfumo imara wa kufadhili shughuli za haki za binadamu nchini. Serikali inaendelea kuthamini mchango wa wadau wanaosaidia kuimarisha utawala wa sheria, haki na maendeleo jumuishi,” amesema Profesa Mkumbo.

Kwa mujibu wa THRDC, mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji, ufikikaji na uendelevu wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya haki za binadamu nchini kupitia mtandao huo.

Mpango huo utatekelezwa kupitia mikakati mitatu mikuu, ikiwemo kuhamasisha rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo na wafadhili wa jadi, kujenga ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kuhamasisha misaada ya kifadhili (philanthropy).

Mkakati mwingine ni kuzijengea uwezo asasi za haki za binadamu za ngazi ya jamii katika maeneo ya maendeleo ya biashara na uwekezaji wenye matokeo chanya (impact investment), ili kuongeza uwezo wao wa kujitegemea kifedha.

Uzinduzi wa mpango huo umefanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 15 wa THRDC, unaowakutanisha wanachama, wadau wa maendeleo, watetezi wa haki za binadamu na viongozi mbalimbali kujadili mustakabali wa ulinzi na utetezi wa haki za binadamu nchini.

THRDC imeeleza kuwa kupitia mpango huo inalenga kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nje vya ufadhili na kujenga mifumo endelevu ya kifedha itakayowezesha asasi na watetezi wa haki za binadamu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mtandao huo umeeleza kuwa uwekezaji katika mifumo endelevu ya ufadhili ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za ulinzi na utetezi wa haki za binadamu zinaendelea kufanyika kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button