RC Kheri atangaza vita dhidi ya utapiamlo Iringa

IRINGA: MKOA wa Iringa umeingia katika hatua nyingine ya mapambano dhidi ya utapiamlo na lishe duni baada ya Mkuu wa Mkoa, Kheri James, kutangaza sera ya uwajibikaji mkali kwa watendaji wote wanaosimamia masuala ya lishe.

Aidha, ameonya halmashauri itakayoshindwa kufikia asilimia 95 ya viashiria vya utekelezaji italazimika kutoa maelezo na kuchukua hatua za haraka za kujirekebisha.

Kauli hiyo imekuja wakati Iringa ikiendelea kupongezwa kwa kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika utekelezaji wa afua za lishe, huku tathmini ya karibuni ikionyesha hakuna halmashauri yenye alama ya njano wala nyekundu katika viashiria vya utendaji.

Akizungumza leo Julai 29, kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe mkoani humo, Kheri alisema mafanikio yaliyopatikana hayapaswi kuwa sababu ya kulegeza juhudi, bali ya kuongeza kasi ya utekelezaji na uwajibikaji.

“Sitaki kuona halmashauri yenye utekelezaji chini ya asilimia 95. Ikitoke hivyo Mkuu wa Wilaya atalazimika kufika na barua ya maelezo kutoka kwa mkurugenzi, afisa lishe na afisa mipango ikieleza kwa nini malengo hayajafikiwa na hatua zilizochukuliwa. Na sitataka kuwaona wahusika kwenye  kikao kinachokuja,” alisema.

Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuwekeza fedha na rasilimali nyingi katika kuboresha lishe, hivyo kila mtendaji anawajibika kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yanayoonekana katika afya na ustawi wa wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema lishe bora ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na taifa, akieleza kuwa taifa lenye wananchi wenye lishe duni hukabiliwa na changamoto za uzalishaji mali, elimu, afya na hata usalama.

“Mtu asiye na lishe bora hawezi kuzalisha ipasavyo, hawezi kufikiri kwa ufanisi na hawezi kuchangia kikamilifu maendeleo ya taifa. Watoto wenye lishe bora wana uwezo mkubwa wa kujifunza na kufaulu shuleni. Hivyo, suala la lishe ni ajenda ya maendeleo, si la sekta ya afya pekee,” alisema.

Aliwahimiza wananchi kutumia kikamilifu neema ya uzalishaji wa chakula uliopo Iringa kwa kula mlo kamili unaojumuisha mboga za majani, matunda, maziwa na vyakula vyenye virutubisho ili kujenga jamii yenye afya na nguvu kazi yenye tija.

Katika sekta ya elimu, Kheri alisema mpango wa chakula shuleni umeendelea kuimarika, huku halmashauri zote zikifikia zaidi ya asilimia 80 ya utekelezaji. Hata hivyo, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari anapata chakula akiwa shuleni.

Alizipongeza halmashauri za Kilolo, Iringa DC na Mufindi kwa kuanzisha mashamba ya shule yanayozalisha mahindi, maharage, mboga mboga na miradi ya ufugaji samaki, hatua aliyoeleza kuwa inaimarisha lishe ya wanafunzi na kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni.

Kwa upande wake, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Anna Nombo, alisema mafanikio ya mkoa yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na wananchi.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo mwitikio mdogo wa wananchi kushiriki maadhimisho ya siku ya afya, hasa katika maeneo ya mijini, hali inayopunguza fursa ya jamii kupata elimu ya lishe na afya.

Alisema baadhi ya vifo vya watoto vinavyotokana na utapiamlo mkali bado vinahusishwa na malezi duni, matumizi ya pombe kupita kiasi kwa baadhi ya wazazi na kuchelewa kuwafikisha watoto katika vituo vya afya.

 

Anna alisema mkoa utaendelea kuhamasisha wazazi kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni, shule zinaanzisha na kuendeleza mashamba ya mazao ya lishe, jamii inapatiwa elimu ya lishe bora na vituo vya kulelea watoto mchana vinaimarishwa ili kuwapa watoto malezi na lishe stahiki.

Aidha, alisema uchunguzi wa hali ya lishe kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano utaendelea kufanyika ili wanaobainika kuwa na changamoto wapatiwe matibabu na ushauri kwa wakati.a

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button