Sabaya atwaa fomu ubunge Arumeru Magharibi

KILIMANJARO: KINYANG’ANYIRO cha ubunge katika Jimbo la Arumeru Magharibi kinazidi kupamba moto baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya kuwa miongoni mwa wanachama 20 wakiwemo wanawake watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Sabaya ambaye hakutaka kabisa kuongea na waandishi wa habari kueleza mipango yake katika jimbo hilo pindi chama kikimteua kwani alifika katika ofisi za CCM jimbo hilo akiongozana na mkewe Jesca Thomas na kusema ‘’anamwachia Mungu afanye kazi yake mbarikiwe sana’’.
Sabaya alikabidhiwa fomu hiyo leo na Katibu wa CCM Arumeru, Camila Kigosi na kufanya kinyang’anyiro hicho katika Jimbo la Arumeru Magharibu kuwa vutanikuvute kufuatia wingi wa watia nia wa nafasi ya ubunge katika Jimbo hilo akiwemo Mbunge wa sasa, Noah Lembris na Mwenyekiti wa CCM Arumeru,Noel Severe
Katika siasa za Mkoani Arusha na Jimbo la Arumeru Magharibi mwaka 2015 alichaguliwa kuwa diwani kata ya Sambasha na mwaka 2016 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha.
Julai 28,2018 Hayati Rais Dk John Magufuli alimteua Sabaya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.