Samia asifu matunda ukodishaji visiwa vidogo

ZANZIBAR; RAIS Samia Suluhu Hassan ametaja manufaa yaliyoanza kupatikana ya uwekezaji kwenye visiwa vidogo nchini na kusema ni pamoja na ajira, kuongezeka kwa mapato, ukuaji wa uchumi wa wananchi na ongezeko la idadi ya watalii.
Alisema hayo wakati akifungua Hoteli ya Nyota Tano ya Cocoon Collection katika Kisiwa cha Bawe ikiwa ni uwekezaji uliofanywa na Waitaliano ambao hadi sasa wameshawekeza kwenye maeneo matatu visiwani humo.
“Mradi huu ni wa watu kuwekezwa na wawekezaji hawa hapa Zanzibar, wamewekeza pia eneo la Nungwi, kwenye Kisiwa cha Prison, hii ni ishara kuwa wameridhika na mazingira ya uwekezaji na sisi kwetu ni faida kwa sababu uwekezaji wa visiwa sasa unaanza kuleta manufaa,” alisema Rais Samia.
Aliongeza: “Uongozi ni kuona mbali, Rais Mwinyi aliona hilo la kukodisha visiwa ili vitunufaishe, zamani uchumi tuliukalia na wavuvi walikalia na tulichokipata pekee ni samaki waliokuwa wakivuliwa na kuuzwa na wavuvi wetu kwenye eneo hilo.”
Alisema ajira zaidi ya 400 zimepatikana katika hoteli hiyo moja lakini pia mradi huo wanalipa kodi, jambo linaloinua uchumi na mapato lakini pia kukuza jina la Zanzibar na muda si mrefu Kisiwa cha Bawe kitatambulika kimataifa na kuleta fursa zaidi kwa nchi.
“Kila jambo jipya lina mambo yake, vilipotangazwa visiwa hivi vinakodishwa tulikuwa wakali, kila kitu kinaonekana hakiwezekani hadi kifanyike, leo nani anajuta kuwa na mradi kama huu? Unainua mapato na kukuza uchumi wetu,” alisema.
Alipongeza pia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kusimamia vizuri uwekezaji kwenye visiwa na Zanzibar kwa ujumla.
Alisisitiza juu ya agizo la Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alilotoa awali wakati akimkaribisha kufungua hoteli hiyo, la kutoa miezi mitatu kuanzia sasa kwa wote waliokodishiwa visiwa vidogo kuviendeleza vinginevyo serikali itawanyang’anya na kuwapa wengine.
“Nimezungushwa kwenye uwekezaji wa hoteli hii, ni miongoni mwa miradi 15 hapa Zanzibar kwenye visiwa vidogovidogo. Nikazie agizo la Dk Mwinyi kwamba wale wote waliopewa visiwa na hawajaviendeleza, ni kwamba wanatudadisi na wanavinadi visiwa vyetu, sasa kabla hawajafanya hivyo tuvichukue baada ya muda huo kupita, tuwape wengine,” alisema.
Alisema mradi huo wa ujenzi wa hoteli katika Kisiwa cha Bawe uliwekwa jiwe la msingi mwaka jana na mwaka huu umekamilika. Alisema hiyo ni hatua ya kupongezwa kwa wawekezaji kutekeleza ndani ya muda mfupi.
“Mradi huu ni wa tatu kuwekezwa na wawekezaji hawa hapa Zanzibar, hii ni ishara kuwa wanaridhika na mazingira ya utawala, wanavutiwa na hali tuliyonayo na urasimu umepungua. Uwekezaji huu ni wa Dola za Marekani milioni 42 si fedha ndogo, wanamradi wa kutengeneza umemejua na mradi wa kusafisha maji bahari kuwa safi,” alisema Rais Samia.
Rais Samia pia alizungumzia mambo yanayoshikamana na uwekezaji huo wa hoteli kwenye visiwa kuwa ni pamoja na uwekezaji kwenye bandari.
Alisema mipango iliyopo sasa na baadaye ni kuendelea kujenga bandari. Alizitaja kuwa ni Bandari ya Malindi inayohusika na kontena na mizigo), Bandari Kavu ya Maruhubi-Fumba na Mkoani Pemba ambazo zinahusika na kontena pekee.
Nyingine ni bandari mpya ya kisasa ya abiria na mizigo ya Maruhubi Mpigaduri na bandari ya kushusha mizigo ya Mangapwani.
“Hayo ni maeneo ya mkakati ya kukuza uchumi wetu kupitia bandari na uchumi wa buluu, bandari hizi hazitaishia hapo, kuna bandari zinatakiwa kukamilishwa ambazo ni pamoja na Bandari Jumuishi ya Mangapwani na zipo zinazofikiriwa kujengwa, Bandari ya Shumba Mjini-Pemba, Micheweni na Ujenzi wa Bandari ya Wete na Ujenzi wa Bandari ya Kizimkazi,” alisema.



