Serikali yalenga kupunguza gharama uzalishaji

DODOMA: WIZARA ya Viwanda na Biashara imeeleza kuwa inaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija, hatua inayolenga kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Imeelezwa kuwa Serikali inaweka mazingira yatakayomwezesha Mtanzania kuongeza faida katika shughuli zake za uzalishaji kwa kuhakikisha anapata miundombinu, nishati, taarifa za masoko na huduma zinazohitajika katika uzalishaji na biashara.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, wakati akieleza kuhusu ushiriki wa wizara hiyo katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanayoendelea jijini Dodoma.

Londo alisema Serikali imepewa maelekezo na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mazingira ya uzalishaji yanaboreshwa kwa makundi yote yanayojihusisha na shughuli za kiuchumi, wakiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi.

“Tuna wajibu wa kumtengenezea mazingira rafiki Mtanzania, awe mkulima, awe mvuvi au awe mfugaji. Kwanza ni kuhakikisha kwamba tunampunguzia gharama za uzalishaji, kwa sababu unapompunguzia gharama maana yake unamhakikishia aongeze faida,” alisema.

Alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko vinavyounganisha maeneo ya uzalishaji na masoko pamoja na viwanda, ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kupunguza gharama zinazobebwa na wazalishaji.

Londo alisema pia Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kusambaza umeme katika vijiji na vitongoji, hatua inayolenga kurahisisha shughuli za uzalishaji na kuongeza uwezo wa wananchi kuanzisha na kuendesha shughuli za kiuchumi.

Alisema uwekezaji huo unaenda sambamba na upanuzi wa mawasiliano kwa kujenga minara katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa za masoko na kufanya maamuzi sahihi kuhusu shughuli zao za uzalishaji.

“Tunapopeleka minara katika vijiji na vitongoji, tunamhakikishia Mtanzania kupata taarifa za uhakika kuhusu soko linavyoenda, ili afanye maamuzi ya uhakika yatakayomletea tija katika shughuli zake za uzalishaji,” alisema.

Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake inaendelea kutoa elimu, ulinzi na huduma mbalimbali kwa wananchi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara na uzalishaji, kuanzia viwanda vidogo, vya kati hadi vikubwa.

Kwa mujibu wa Londo, Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni muhimu kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuwa mazao yanayotokana na sekta hizo ni bidhaa zinazoweza kuingia katika masoko na wakati huo huo kuwa malighafi kwa ajili ya viwanda.

Alisema wizara hiyo imeshiriki katika maonesho hayo ikiwa na lengo la kuhamasisha na kuwezesha ongezeko la thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia usindikaji na utengenezaji wa bidhaa.

“Kwa hiyo mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanaweza kutumika kama malighafi kwa ajili ya viwanda, lakini pia ni bidhaa zinazoingia katika soko la biashara,” alisema.

Alisema taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zimeshiriki katika Banda la Tatu la maonesho hayo, ambako wananchi wanapata huduma na elimu mbalimbali zinazohusiana na biashara na viwanda.

Alitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Alisema BRELA inatoa huduma zinazohusisha usajili wa kampuni na majina ya biashara pamoja na huduma nyingine za kuwawezesha wananchi kuanzisha na kukuza shughuli zao za kibiashara.

Kwa upande wake, TBS, FCC na SIDO zinaendelea kutoa huduma na elimu kwa wafanyabiashara na wazalishaji kwa lengo la kuongeza ushindani, ubora wa bidhaa na kujenga mnyororo wa thamani.

  1. Londo aliwataka Watanzania kutembelea Banda la Tatu ili kupata huduma na elimu zinazotolewa na taasisi hizo, akisisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi kushiriki katika biashara, uzalishaji na ujenzi wa uchumi wa Taifa kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button