Serikali yashauriwa kukabiliana na ushirikina, kamari

SERIKALI imetakiwa kuongeza juhudi za kukabiliana na ongezeko la imani za kishirikina nchini kwa sababu imani hizo zinavuruga jitihada kubwa na muhimu za serikali kuboresha elimu nchini.

Aidha, serikali imeshauriwa kuliangalia upya suala la uchezaji kamari lililozagaa nchini kwa sababu michezo hiyo ni utapeli, na inasaidia kujenga imani kuwa watu wanaweza kuishi, na kuendesha maisha yao, bila kufanya kazi bali kwa kushinda katika nyumba za kucheza kamari.

Ushauri huo kwa serikali kuhusu imani za ushirikina na michezo ya kamari ulitolewa mwishoni mwa wiki wakati wa sherehe ya Mahafali ya Uhitimu wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (MJKN) ya Mbezi Beach, Dar es Salaam.

“Jambo la ajabu ni kwamba kiwango cha elimu yetu kinaongezeka. Lakini juhudi hizo zinavurugwa na ongezeko kubwa la imani za kishirikina. Tunao watu wengi sasa wenye shahada za uzamivu (PhD) lakini vile vile tunao wajinga wengi zaidi sasa. Profesa wa Fizikia ama Kemia anakwenda kupiga ramli kwa mganga,” Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shule ya MJKN, Jenerali Ulimwengu.

Ulimwengu aliongeza: “Imekuwa ni kama kazi bure. Tunafanya jitihada kubwa za elimu, lakini ushirikina unadumaza jitihada hizo…ni lazima kama jamii, tutafute namna ya kuondokana na imani ambazo sasa zimesambaa miongoni mwa watu wetu, ndani ya jamii yetu.”

“Imani hizi zinaguguna kila tunachowafundisha watoto wetu, zinaua jamii yetu. Huku chini, tunalima vizuri na kuvuna vizuri, lakini tunapoweka mazao yetu kwenye maghala ya kuyahifadhi, yanatafunwa na mdudu huyu anaitwa ushirikina.”

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya MJKN alikuwa akizungumza akimkaribisha mgeni rasmi katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba.

Ulimwengu alisema imani hizo ndizo pia zinawaingiza watu katika shughuli za kamari za kubashiri.

“Watu wanadanganywa kupoteza pesa kidogo waliyonayo katika shughuli isiyoweza kuzalisha…ni uongo mkubwa, ni matapeli wakubwa hawa, wanadanganya vijana wetu…redio za FM na viduka vya ‘betting’ ndiyo yamekuwa maisha ya vijana wetu.”

“Mitaani, sisi hapa, tunahangaika kutoa elimu, na watoto wanayo hamu ya kupata elimu, lakini wakikua kidogo tu wanaaza kupumbazwa kwa kudanganywa kuwa wanaweza kupata pesa, kutajirika bila kufanya kazi.

“Watu wanaishi kwa kiini macho tu… kweli hii ni hadithi kamili ya wajinga ndio waliwao…watu wanaamini ndoto za mchana kuwa unaweza kuishi bila kufanya kazi na bado ukawa tajiri,” alisema Ulimwengu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mgumba alikubaliana na Ulimwengu na kusema kuwa imani za ushirikina zimeota mizizi katika jamii ya Watanzania.

“Imani hizo zinaleta uhasama ndani ya jamii. Imani hizi zinavuruga amani katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu,” alisema, akitoa mfano wa Mkoa wa Songwe ambako alikuwa mkuu wa mkoa kabla ya kuhamishiwa Tanga.

“Kule tulikuwa na watu wanaitwa lambalamba, wanaleta chuki kubwa sana ndani ya jamii,” alieleza Mgumba.

Mkuu huyo wa mkoa pia aliwashauri Watanzania kuongeza ari na kasi katika kushiriki mijadala ya matatizo katika sekta ya elimu ambayo imeanzishwa na serikali inayotafuta namna ya kutunga sera mpya ya elimu.

“Huu ndiyo wakati wetu kushiriki katika mijadala hiyo, siyo kwenye mijadala ya demokrasia pekee yake, lakini katika mijadala ya kutafuta changamoto nyingine katika jamii yetu zikiwemo za elimu, za matatizo ya ajira, mfumuko wa bei, usalama wetu…hapa Dar sasa kuna Panya Road na hata rushwa,” alieleza Mgumba.

Wanafunzi 47 walihitimu katika sherehe hiyo, tayari kuendelea na safari yao ya elimu kwenye ngazi ya sekondari.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x