Sh bilioni 1.2 kusaidia watoto wenye magongwa ya moyo

GEITA: KIASI cha Sh bilioni 1.2 kimetengwa kwa kipindi cha miaka mitatu kusaidia matibabu ya watoto 300 wenye magonjwa ya moyo nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa watoto ambao familia zao zitashindwa kumudu matibabu.
Kupitia makubaliano yaliyosainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya Geita Gold Mining Limited (GGML) mkoani Geita, kati ya GGML na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kampuni hiyo itatoa takribani Sh milioni 400 kila mwaka kusaidia matibabu ya watoto 100 wenye matatizo ya moyo, hivyo kufikisha jumla ya takribani watoto 300 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Ushirikiano huo umefikiwa kwa uratibu wa Global Medicare ya jijini Dar es Salaam, ambayo imekuwa ikiunganisha wadau na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo nchini.
Makubaliano hayo yanaongeza nguvu katika juhudi za Serikali na wadau wa sekta binafsi kupanua fursa za matibabu ya moyo kwa watoto, hususan wale wanaohitaji huduma za kibingwa ikiwemo upasuaji na tiba maalumu za kurekebisha matatizo ya moyo.
Akizungumza katika hafla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, amesema uamuzi wa kampuni kuunga mkono mpango huo ulifikiwa baada ya kupitia mchakato wa kina wa tathmini unaotumika katika miradi yote ambayo kampuni inaombwa kuisaidia.
Amesema baada ya uongozi wa kampuni kupata maelezo kuhusu mpango huo, historia ya ushirikiano uliokuwapo pamoja na matokeo yaliyopatikana katika kusaidia watoto na kuimarisha huduma za moyo, kampuni iliona umuhimu wa kuwekeza katika mpango huo.
“Tunatazamia ushirikiano wa miaka mitatu. Ni watoto 100 kwa mwaka na takribani Sh milioni 400 kwa mwaka. Tunatarajia ushirikiano huu kuwa wa mafanikio na tunatumaini utaendelea hata katika siku zijazo,” amesema Suryaningrat.

Amesema uamuzi huo si mafanikio ya mtu mmoja bali ni matokeo ya kazi ya pamoja ya timu mbalimbali zilizoshiriki kuwasilisha, kutathmini na kufanikisha mpango huo, akizishukuru JKCI, Global Medicare pamoja na watendaji wa GGML waliohusika katika mchakato huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dkt. Peter Richard Kisenge, amesema msaada huo una umuhimu mkubwa kwa sababu utagusa moja kwa moja maisha ya watoto wanaohitaji huduma za haraka za moyo.
Amesema magonjwa ya moyo kwa watoto yanaendelea kuwa changamoto inayohitaji ushirikiano mpana, huku baadhi ya watoto wakihitaji upasuaji, wengine taratibu maalumu za kuziba matundu ya moyo na wengine wakihitaji dawa pamoja na ufuatiliaji wa kitabibu.
Dkt. Kisenge amesema mchango huo wa GGML haupaswi kuangaliwa kama msaada wa fedha pekee, bali kama uwekezaji katika kuokoa maisha na kurejesha matumaini kwa watoto na familia zao.
“Huu si msaada wa pesa tu. Huu ni msaada unaokwenda kuokoa maisha. Mmeenda kutimiza matumaini ya watoto ambao wanakwenda kujenga Taifa la Tanzania la kesho,” amesema Dkt. Kisenge.
Amesema watoto wengi wanaohitaji huduma hizo hutoka maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Kanda ya Ziwa, na hivyo msaada huo utakuwa na manufaa makubwa kwa familia ambazo bila kuwepo kwa ushirikiano wa aina hiyo zingekabiliwa na changamoto ya kupata matibabu ya kibingwa kwa watoto wao.
Dkt. Kisenge ameishukuru GGML kwa niaba ya Mh Rais Dtk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Afya, JKCI, Wazazi na familia za watoto watakaonufaika, akisema kampuni hiyo imechagua kuwekeza katika eneo ambalo matokeo yake yanapimwa moja kwa moja kwa maisha yanayookolewa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel, amesema magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa changamoto kubwa, huku JKCI ikiwa imejijengea nafasi muhimu katika utoaji wa huduma za kibingwa za moyo kwa Watanzania pamoja na wagonjwa kutoka nchi nyingine za ukanda huu.
Amesema wagonjwa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Zambia, Malawi, Kenya na Uganda wamekuwa wakitegemea huduma za JKCI, hali inayoonesha nafasi ambayo Tanzania imejenga katika utoaji wa huduma za kibingwa za moyo.
Mollel amesema pia kuna wagonjwa wengi wanaotoka katika maeneo yenye shughuli za migodi, hivyo ni muhimu kuendelea kuongeza elimu ya afya, uelewa kuhusu kinga, uchunguzi wa mapema na upatikanaji wa matibabu kwa wakati.
Amesema uamuzi wa GGML kutoa mchango huo ni hatua kubwa katika kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo na unadhihirisha namna sekta binafsi inaweza kushirikiana na taasisi za Serikali katika kuokoa maisha.



