Shule zatakiwa kuweka kipaumbele Tehama

KAGERA: Serikali imezitaka shule nchini kuweka kipaumbele kwenye mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa wanafunzi wao ili kwenda sanjari na dunia ya sasa ya utandawazi na teknolojia inayokua kwa kasi.

Serikali imeeleza kwa dunia ya sasa teknolojia inakwenda kwa kasi kubwa hivyo shule zinapaswa kuwa na miundombinu bora ya wanafunzi wake kujifunza TEHAMA huku ikiipongeza shule ya Bunazi Green Acres iliyoko mji mdogo wa Bunazi Kata ya Kassambya wilayani Misenyi kwa kuwa mfano kwenye eneo la mafunzo ya TEHAMA.

Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, Phocus Rwegasira, wakati wa mahafali ya 10 ya shule hiyo ya Bunazi Green Acres iliyoko mji mdogo wa Bunazi Kata ya Kassambya wilayani Misenyi yaliyofanyika shuleni hapo ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.

Alisisitiza kuwa mafunzo ya teknolojia ni muhimu kwani dunia inakwenda kwa kasi kwenye eneo hilo huku akisisitiza pia umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, walimu na jamii katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na malezi yanayowaandaa kuwa viongozi na wataalamu wa baadaye.

Alisema pamoja na shule hiyo kuweka miundimboinu bora na ya kisasa lakini mafanikio ya mwanafunzi hayawezi kutenganishwa na juhudi za walimu, wazazi na uongozi wa shule, hivyo kila upande unapaswa kutekeleza wajibu wake kwa umakini.

Rwegasira pia aliwahimiza wahitimu kuwa na nidhamu, bidii na kujituma katika masomo yao ya ngazi zinazofuata, akiwataka kutumia fursa za elimu kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha, aliwataka wazazi kuendelea kuwa karibu na watoto wao, kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma na kuwajengea misingi mizuri ya maadili.

Katika hafla hiyo, Rwegasira alikabidhi vyeti kwa baadhi ya wahitimu, huku akipongeza uongozi wa Bunazi Green Acres kwa kutimiza miaka 10 ya mahafali na kuendelea kutoa mchango katika sekta ya elimu nchini.

Mkurugenzi wa Shule ya Bunazi Green Acres, Jackline Rushaigo, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, wazazi na jamii katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na malezi yenye misingi ya maadili.

Alisema mafanikio yaliyofikiwa na shule hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja za walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wa elimu.

Aliwapongeza wanafunzi waliohitimu kwa hatua waliyofikia na kuwataka kuendelea kuwa na nidhamu, bidii na kujituma katika masomo yao ya ngazi zinazofuata.

Aidha, aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuendelea kuiamini shule hiyo na kushirikiana na uongozi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kukua kitaaluma na kimaadili.

Mkuu wa shule hiyo, Geoffrey Moses alisema shule hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka 10 iliyopita imepata mafanikio makubwa kwani wanafunzi wake wote wamekuwa wakipata daraja A katika matokeo ya mitihani ya kitaifa inayotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA).

Alisema shule imejitahidi kuboresha miundombinu yake kwa kujenga majengo sita ya madarasa yenye vyumba 25 vya kujifunzia na imejanga maabara ya kisasa ya TEHAMA yenye huduma za mtandao kwaajili ya mafunzo kwa vitendo.

Alisema shule imejitahidi kujenga maktaba yenye vitabu vingi vya kiada na vya ziada na mabweni sita yenye vitanda kwa kila mwanafunzi na kwamba mazingira hayo ndiyo yameiwezesha shule kutoa huduma bora na matokeo mazuri kila mwaka.

“Tunajivunia kwamba miaka yote 10 tangu shule ianze tumefanya vizuri kitaaluma tumeshatoa wanafunzi 500 kwa miaka yote 10 na muda wote huo shule imekuwa ikipata wastani wa alama 251 ambayo ni darasa A bora,” alisema

Aidha, alisema mafanikio ya shule hiyo yametokana na juhudi kubwa za walimu wake nidhamu ya wanafunzi na ushirikiano mkubwa wa wazazi na serikali kuanzia ngazi ya kata hadi nagzi ya Wizara.

“Mwaka huu tuna wahitimu 64 wa darasa la saba ambao tunaamini wataendeleza historia yetu nzuri ya kitaaluma kwasababu wameandaliwa vizuri sana,” alisema

Aidha, Mkuu huyo wa shule alisema katika kutambua ulimwengu unavyokwenda kwa kasi kwenye teknolojia, shule imeanzisha maabara ya TEHAMA yenye mtandao ili kuwapa wanafunzi ujuzi wa kompyuta kwa vitendo.

“Wanafunzi wetu wanajivunia kutumia teknolojia kwa kujiamini na kwa ubinifu hivyo tunaamini ujuzi huu utawaandaa kushindana na kufanikiwa katika dunia ya sasa,” alisema mwalimu Mosses

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button