Tanzania kupanua huduma za moyo Comoro

DAR ES SALAAM: UHITAJI mkubwa wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini Comoro umeibua fursa kwa Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupanua huduma zake katika nchi hiyo.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Dk Salim Hamad, amesema uhitaji huo umeonekana wazi baada ya JKCI kufanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo katika kisiwa cha Anjouan, ambapo uongozi wa kisiwa hicho umeomba taasisi hiyo kuingia mkataba wa kuendelea kutoa huduma hizo.

Dk Hamad amesema ombi hilo ni ishara ya kuaminiwa kwa wataalamu wa Tanzania na fursa ya kuimarisha ushirikiano wa afya kati ya nchi hizo mbili.

Ametoa rai hiyo alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

“Nilifurahi nilipokutana na uongozi wa kisiwa cha Anjouan na kuniomba niwajulishe kuwa wanataka tuingie nao mkataba wa kufanya kambi za matibabu. Hii ni hatua kubwa kwa nchi yetu katika kutoa huduma bingwa za matibabu ya moyo,” amesema Dk Hamad.

Kwa upande wake, Dk Kisenge amesema mwitikio mkubwa wa wananchi wakati wa kambi iliyofanyika Oktoba mwaka jana unaonesha kuwa kuna mahitaji makubwa ya huduma za moyo nchini Comoro.

Amesema JKCI inaandaa mkakati wa kuitangaza taasisi hiyo nchini Comoro ili wananchi wengi zaidi wafahamu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na kupata matibabu bila kulazimika kusafiri mbali.

“Tunaandaa mkakati wa kuitangaza JKCI nchini Comoro ili tuweze kuwasaidia wananchi wa Comoro kufahamu zaidi huduma tunazozitoa na kuwapunguzia adha ya kuzifuata huduma hizi mbali na nchi ya Comoro,” amesema.

Dk Kisenge amesema hatua hiyo inaweza kuongeza wigo wa huduma za kibingwa zinazotolewa na Tanzania nje ya nchi, huku ikiimarisha zaidi uhusiano wa Tanzania na Comoro katika sekta ya afya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button