Tanzania, Uturuki zaimarisha ushirikiano sekta ya afya

DAR ES SALAAM: BALOZI wa Uturuki nchini Tanzania, Bekir Gezer, amesema uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki unaendelea kukua na kuimarika katika maeneo mbalimbali, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuleta fursa na manufaa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam baada ya Chuo Kikuu cha Ankara na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kwa ushirikiano wa Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TIKA), kusaini makubaliano ya kuanzisha Kitengo Maalum cha Huduma za Usingizi kwa Watoto Wakati wa Matibabu ya Meno (Pediatric Dental Sedation Unit).
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Balozi huyo amesema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza uhusiano ya Tanzania na Uturuki katika maeneo mbalimbali, hususan sekta ya afya.
Amesema kauli mbiu ya ushirikiano huo ni “Tufanye kazi pamoja, tushiriki pamoja,” akieleza kuwa Uturuki iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kila eneo litakalokuwa na manufaa kwa wananchi.

“Uturuki iko tayari kushirikiana katika kila eneo. Hii ni mlango wa matumaini na mustakabali bora. Mradi huu utakuwa na manufaa kwa kila mtu,” amesema.
Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa kitengo hicho ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa watoto, huku akisisitiza umuhimu wa nchi hizo mbili kuendelea kubadilishana uzoefu, maarifa na utaalamu katika sekta ya afya.
Kwa mujibu wa Balozi huyo, ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki utaendelea kupanuka katika maeneo mbalimbali, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya safari ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo.
“Mahusiano yanaendelea kukua. Tunataka kuona uhusiano ukiendelea katika maeneo yote. Ushirikiano utaongezeka na kustawi,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema wamekuwa wakishirikiana na wadau hao katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya afya.
Amesema moja ya maeneo makubwa ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Ankara na TİKA ni kuanzishwa kwa Kliniki ya Watoto yenye Matatizo ya Kinywa na Meno inayohitaji huduma za usingizi wakati wa upasuaji.
Amesema kabla ya kuanzishwa kwa huduma hiyo, huduma ya kuwafanyia watoto wenye changamoto za kinywa na meno upasuaji kwa kutumia dawa za usingizi haikuwepo kwa kiwango kikubwa nchini Tanzania.

“Kwa kawaida, mgonjwa anayefanyiwa huduma ya meno hupatiwa dawa ya kupunguza maumivu inayodungwa kwenye eneo husika. Hata hivyo, kuna baadhi ya watoto ambao hawawezi kuvumilia au kushirikiana wakati wa matibabu. Watoto wadogo wanaweza kuogopa sindano au kushindwa kukaa katika hali inayomwezesha daktari kutoa huduma ipasavyo,”
“Pia, kuna watoto wenye mahitaji maalumu ambao wanahitaji huduma hii kwa usalama na ufanisi zaidi. Kupitia ushirikiano huu, tumeanzisha huduma maalumu ambapo mtoto anaandaliwa, anapatiwa dawa za usingizi chini ya uangalizi wa wataalamu, anafanyiwa upasuaji na kisha anaendelea kufuatiliwa hadi anapoamka salama,” amesema Kamuhabwa.
Kamuhabwa amesema huduma hiyo ni muhimu kwa sababu inahudumia watoto ambao awali ilikuwa vigumu kuwapatia huduma za meno kutokana na changamoto zao. “Katika kufanikisha huduma hii, TİKA na Chuo Kikuu cha Ankara vimetusaidia kwa namna mbalimbali,´ameongeza Kamuhabwa.
Amesema MUHAS walipeleka madaktari bingwa wa kinywa na meno, madaktari bingwa wa usingizi, wataalamu wa maabara pamoja na wauguzi katika Chuo Kikuu cha Ankara kwa ajili ya mafunzo kutoka kwa maprofesa na madaktari wa Uturuki.

Prof Kamuhabwa amesema baada ya mafunzo hayo, wataalamu kutoka Uturuki walikuja Tanzania na kutoa mafunzo kwa wataalamu ambapo walifanya majaribio na baada ya kujiridhisha kuwa wataalamu walikuwa tayari, walianza kutoa huduma.
“Aidha, kupitia TİKA tumepata vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya huduma hii. Kwa sasa vifaa tunavyo na huduma imeanza kutolewa tangu mwezi Mei mwaka huu. Katika kipindi hicho, tayari tumeshawahudumia watoto 27,” amesema Prof Kamuhabwa.

Amesema moja ya maeneo muhimu ni kuhakikisha wanawapa mafunzo wataalamu wengi zaidi, kuongeza vifaa na pia kupanua eneo la kutolea huduma ili tuweze kuwahudumia watoto wengi zaidi.
“Eneo la pili la ushirikiano ni huduma za dharura. Kama tunavyojua, paramedics ni wataalamu ambao si madaktari, lakini wamefundishwa kutoa huduma muhimu za awali kwa wagonjwa wa dharura. Kwa mfano, ajali ya barabarani inapotokea, mgonjwa anapookolewa anahitaji kushughulikiwa kwa namna sahihi,”



