TIB kuongeza ufadhili nishati safi vijijini

BENKI ya Maendeleo ya TIB imeahidi kuongeza juhudi katika kusaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini na maeneo mengine ambayo bado hayajafikiwa kwa urahisi na huduma hiyo. Ahadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Deogratius Kwiyukwa, wakati wa mjadala wa jopo kuhusu nishati safi ya kupikia uliofanyika Kizimkazi, Zanzibar.
Kwiyukwa amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wengine katika kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya nishati safi ya kupikia, hasa katika jamii ambazo bado zinategemea kuni na mkaa.
“Lengo letu ni kufanya kazi na Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wengine ili kuhakikisha ufadhili unapatikana kwa miradi ya kupikia safi na kwamba rasilimali zinawafikia jamii zinazozihitaji zaidi,” alisema.SOMA: Serikali yataka wanahabari kuhamasisha nishati safi ya kupikia

Amesema TIB inatekeleza majukumu matatu katika kusaidia miradi ya maendeleo, yakiwamo kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa miradi ya muda wa kati na mrefu, kuandaa miradi inayoweza kupata ufadhili na kusimamia mifuko mbalimbali ya maendeleo kwa niaba ya taasisi husika.
Kwa mujibu wa Kwiyukwa, baadhi ya mifuko inayosimamiwa na benki hiyo inalenga kusaidia juhudi za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na miradi ya nishati taka.Amesema usimamizi wa mifuko hiyo unalenga kuhakikisha miradi inayofadhiliwa inatekelezwa kwa ufanisi na kuwafikia walengwa.
“Tanzania imepiga hatua katika kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi wanaoendelea kutegemea kuni na mkaa,” alisema. Amesema Serikali ina lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wadau wengine ni muhimu katika kuongeza uwekezaji kwenye sekta hiyo. Kwa mujibu wa Kwiyukwa, uwekezaji katika nishati safi ya kupikia pia utasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuhifadhi mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kijani.


