‘Ugatuzi wa madaraka muhimu kufanikisha Dira 2050’

DODOMA: NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (anayeshughulikia afya), Jafar Seif, amesema ugatuzi wa madaraka ni miongoni mwa misingi muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuziimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akifungua mkutano wa mwaka wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa(TaOA) Dk Seif alisema kufikiwa kwa malengo ya Dira 2050 kutategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa Serikali za Mitaa kusimamia na kutekeleza mipango ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika maeneo yao.

Alisema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kiutendaji pamoja na usimamizi wa fedha za umma, ikiwemo utaratibu wa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo moja kwa moja katika taasisi za Serikali za ngazi za chini.

Taasisi zinazofikiwa na utaratibu huo ni pamoja na shule, zahanati, ofisi za kata na vijiji, hatua inayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia alisema Serikali za Mitaa zina nafasi muhimu katika kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa kutokana na kuwa ndizo zilizo karibu zaidi na wananchi na zinaelewa kwa undani mahitaji na changamoto zinazowakabili.

“Fursa ya kufikia Dira ya Taifa 2050 inahitaji Serikali za Mitaa zenye uongozi bora na uwajibikaji, mipango madhubuti ya maendeleo na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma,” amesema.

Aidha, Dk Seif amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji katika ngazi mbalimbali za Serikali.

Alisema kuimarishwa kwa mifumo ya kiutendaji katika Serikali za Mitaa kutasaidia kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa tija na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button