Uwekezaji Bandari ya Mtwara wafungua fursa kiuchumi

MTWARA: ONGEZEKO la shehena na meli katika Bandari ya Mtwara limefungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi, madereva, wafanyabiashara na mawakala wa usafirishaji, huku maboresho ya miundombinu yakiiwezesha bandari hiyo kuhudumia mizigo mikubwa kwa mwaka mzima.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Hekima Ngezi alisema bandari hiyo iliyoanzishwa mwaka 1950 imeboreshwa kwa kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na shehena, tofauti na awali ilipotegemea zaidi msimu wa karanga na baadaye korosho.
Alisema gati zimeongezwa kutoka tatu hadi nne, huku moja likiwa na urefu wa mita 300 na kina cha maji cha mita 13, hali inayowezesha meli kubwa kutia nanga na kupakia au kushusha mizigo kwa ufanisi.
“Mpaka sasa, Bandari ya Mtwara inahudumia shehena ya mafuta, korosho, makaa ya mawe, mbaazi na saruji na tunahudumia magari makubwa. Kuanzia Februari mwaka huu hadi sasa, tumehudumia meli 23 na magari 6,390,” alisema.
Ngezi alisema saruji kutoka Kiwanda cha Dangote husafirishwa kwenda Zanzibar, Comoro na Msumbiji kwa ajili ya miradi ya Gesi Asilia (LNG).
Alisema serikali inaendelea kujenga gati jipya Kisiwa Mpangawe/Kisiwa Mgao, lenye urefu wa mita 300 na kina cha maji cha mita 15, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 44 na linatarajiwa kukamilika mwakani.
Kwa mujibu wa Ngezi, gati hilo litahudumia mizigo yenye vumbi, ikiwamo saruji na makaa ya mawe, huku eneo hilo likiwa na uwezo wa kuhudumia tani 100,000 kwa pamoja.
Alisema Bandari ya Mtwara ni kiungo muhimu katika Ushoroba wa Kusini unaounganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma hadi Bandari ya Mbamba Bay, ambako mizigo inaweza kusafirishwa kwenda Malawi na nchi nyingine jirani.
Kwa wananchi, ongezeko la shughuli bandarini limekuwa chanzo cha kipato. Mama lishe, Rehema Mputa alisema biashara yake imeimarika na kumwezesha kumsomesha mtoto wake hadi kidato cha nne, huku pia akiwekeza katika kilimo.
Bodaboda, Issa Mchika alisema ongezeko la magari ya mizigo na mafuta limeongeza abiria na kipato, tofauti na zamani ambapo shughuli nyingi zilitegemea msimu wa korosho.
Kwa upande wake, Wakala wa Baruti International Limited, Abdulrahman Upete alisema uwekezaji katika mitambo na miundombinu umeongeza ufanisi wa Bandari ya Mtwara na kupunguza mzigo kwa Bandari za Dar es Salaam na Tanga.



