Vijana 57 watia nia udiwani, ubunge Chato

VIJANA wapatao 57 kutoka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Chato mkoani Geita wameonesha nia ya kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali Uchaguzi Mkuu 2025.

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Chato, Frank Kuzenza ametoa taarifa hiyo Juni 23 kwa waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Baraza la Vijana la Wilaya.

Kuzenza amesema miongoni mwa vijana hao ni wajumbe wa baraza la vijana, viongozi pamoja na wanachama wa UVCCM wilayani humo, hali inayoashiria mwamko wa vijana katika kuwania uongozi.

Amesema taarifa ya vijana wenye nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu Oktoba 2025 zinatolewa kuanzia ofisi za UVCCM kata na wilaya na mchakato unaendelea kung’amua vijana wenye nia na uwezo.

“Mwaka huu tumeona kwa kiasi kikubwa vijana wamehamasika, na wamehamasika kwa sababu sisi UVCCM Chato tumekuwa tukipita na kuwahamasisha vijana waingie kwenye vyombo vya maamuzi,” amesema.

Ameema uongozi wa UVCCM wilayani Chato umejipanga kuwaunga mkono, kuwasemea na kuwatetea vijana wenye uwezo na sifa ya kuwa viongozi ili wapewe fursa ya kupeperusha bendera ya CCM.

“Naamini wapo vijana wanazo hoja za msingi ambazo wakienda kwenye uchaguzi wa ndani wa chama wataeleweka,” amesema Kuzenza.

Amesema CCM inafahamu nafasi ya vijana mahiri, wenye uwezo na utayari wa kwenda kusimamia mambo mbalimbali ili kuleta maendeleo kwenye kata zao, kwani bado vijana wana nguvu ya kulitumikia taifa.

Amewataka vijana wilayani Chato kuachana na propaganda zinazoweza kuvuruga uchaguzi ndani na nje ya chama, badala yake wajiandae kutumia kikamilifu haki ya kikatiba kwa kugombea au kupiga kura.

Katibu wa CCM Wilaya ya Chato, Dotto Mazuri amewasisitiza vijana wanapowania na kukosa  wasikate tamaa badala yake waendelee kujaribu mara kwa mara ili wanyanyuke na kukua zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button