Vikundi vya michezo kunufaika mikopo asilima 10

MOROGORO: MBUNGE wa Jimbo la Mvomero, mkoani Morogoro, Sara Msafiri, amevitaka vikundi ambavyo vitashiriki kwenye tamasha la michezo kwenye jimbo hilo vitakuwa vya kijasiriamali na vitasaidiwa usajili ili vipate kunufaika na fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Msafiri amesema hayo wakati akizindua Tamasha la Sara Festival litakalohusisha mashindano ya mpira wa miguu ,ngoma za asili na riadha kwa kushirikisha vijiji vyote 130 vilivyopo katika kata 30 katika halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema lengo la tamasha hilo si tu kuibua vipaji vya vijana bali ni njia sahihi ya kuhimiza vijana kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa vijana ,wanawake na makundi maalumu.

“Kikundi cha ngoma , timu za mpira wa miguu pamoja na riadha za kutoka vijiji vyote 130 vilivyopo ndani ya wilaya yetu kitakachoshiriki pia kitageuzwa kuwa ni cha ujasiriamali na kitasaidiwa kusajiliwa na halmashauri kinufaike na asilimia 10,” amesema Msafiri.

Msafiri amewataka washiriki wa tamasha hilo kuhakikisha wanatumia fursa ya kujitangaza vizuri kwa sababu litakuwa jukwaa kubwa litakalofuatiliwa na watu wengi na hivyo kuwafungulia njia ya kushiriki matamasha ya kitaifa na kimataifa

Mbunge huyo ametolea mfano kuwa ngoma za kabila la Waluguru zimekuwa zikiwavutia watu wengi kutokana na kuendelea kudumisha mila zenye kusisitiza maadili, desturi na utamaduni wa Mwafrika

Naye, Mwenyekiti wa Chimbuko Band na Kikundi cha Ngoma ya Asili ya Mdundiko kutoka Kijiji cha Tangeni, John Mkude amesema kikundi hicho kinazaidi ya miaka 50 na kimekosa kuungwa mkono wa ufadhili kutoka kwa wadau na kujikuta wakibaki katika hali duni ya kiuchumi.

Mkude amesema kikundi hicho kina wanachama 37 na kinafanya shughuli za utumbuizaji kwenye halfa za kijadi asili na kuingiza kipato kwa ajili ya kugawana ili kukidhi mahitaji ya kifamilia pekee.

Kwa upande wake Msanii na Mweka hazina wa kikundi hicho, Benard Shaban amempongeza Mbunge kwa kuanzisha tamasha hilo ambalo litawasadia wasanii wa ngoma za asili kutangaza vipaji vyao na kwa makundi mengine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button