Viongozi Moshi Vijijini watakiwa kushirikiana

KILIMANJARO; Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu, amewataka viongozi wa chama na serikali kuendelea kushirikiana na kujenga umoja badala ya kuweka mbele tofauti zao, akisema mshikamano wa viongozi ni muhimu katika kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Mahanyu amesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kifuni, Kata ya Kibosho Magharibi, wilayani Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, ambapo alisema chama kinapaswa kuwa na utamaduni wa kuwaunganisha viongozi na kuwapa nafasi ya kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Amesema mabadiliko ya viongozi yasiyokuwa na msingi wa utendaji yanaweza kuvuruga mipango ya maendeleo, kwa kuwa kiongozi anayeondolewa kabla ya kukamilisha mipango yake huacha kazi zikiwa hazijakamilika.

“Hatubadilishi viongozi kama mashati. Kiongozi akishapanga mipango, hajamaliza tunamtoa. Kwa kufanya hivyo, tunajenga mdororo kwenye maendeleo,” alisema Mahanyu.

Katika kuonesha umuhimu wa umoja na ushirikiano miongoni mwa viongozi, Mahanyu aliwaunganisha mikono Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, na Diwani wa Kata ya Kibosho Magharibi, Deo Mushi, kama ishara ya mshikamano na dhamira ya viongozi hao kuungana na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kuleta maendeleo katika jamii.

Mahanyu amesema kitendo hicho ni mfano wa namna viongozi wanavyopaswa kushirikiana, kuondoa tofauti zao na kuweka mbele maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo yanahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa viongozi, chama, serikali na wananchi.

Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kupewa ushirikiano na wananchi pamoja na chama ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Akimzungumzia Mbunge wa Moshi Vijijini, Makoi, Mahanyu amesema anaamini kuwa ushirikiano wa viongozi na wananchi utamwezesha kutekeleza mipango yake, hususan katika masuala ya miundombinu, barabara na miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo.

Mahanyu pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaamini viongozi wanaoonesha uwezo na matokeo katika utendaji wao, akisema jambo la msingi linapaswa kuwa kazi wanazofanya kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Vijijini, Makoi, aliwataka wananchi kuungana na kushirikiana katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo hilo.

Nae, Diwani wa Kata ya Kibosho Magharibi, Deo Mushi, amesisitiza umuhimu wa mshikamano kati ya wananchi na viongozi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi katika kata hiyo.

Mushi amesema maendeleo hayawezi kupatikana kwa juhudi za mtu mmoja, bali yanahitaji ushirikiano wa viongozi na wananchi katika kubaini changamoto, kupanga vipaumbele na kusimamia utekelezaji wa miradi.

Amesema wananchi wanapaswa kuendelea kuwaunga mkono viongozi wao na kutoa ushirikiano katika shughuli za maendeleo, huku viongozi wakihakikisha wanakuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button