‘Vyombo vya dola vitakuwa macho Uchaguzi Mkuu’

DODOMA — Rais Samia Suluhu Hassan, ametahadharisha kuwa vyombo vya dola vitakuwa macho kipindi chote cha uchaguzi kwa ajili ya kusimamia sheria, amani na utulivu wa nchi.
Akihutubia leo Juni 27, 2025, wakati wa kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 jijini Dodoma, Rais Samia amesema Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu unakuwa huru, wa haki, na unaofanyika kwa mazingira salama.
“Narudia kusisitiza: Serikali na vyombo vyake vitakuwa macho kipindi chote cha uchaguzi. Tutasimamia sheria na kuhakikisha nchi inabaki kuwa na amani na utulivu,” amesema Rais Samia kwa msisitizo.
Aidha, Rais amewatahadharisha wanaotafuta nafasi za kisiasa kwa malengo binafsi au kwa njia zisizofuata sheria. Amewataka wagombea wote kuzingatia taratibu, kanuni na maadili ya uchaguzi, huku akitoa mfano wa viongozi wa kiserikali watakaosimamia kwa ukaribu zoezi hilo.
“Msisahau – Chalamila yupo,” amesema kwa sauti ya mzaha iliyozua kicheko bungeni, akimaanisha kwamba wasimamizi wa uchaguzi hawatakuwa na mzaha na uvunjaji wa sheria.
Amesisitiza kuwa uchaguzi ni zoezi la kikatiba na muhimu kwa maendeleo ya demokrasia, linalowapa wananchi nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa misingi ya sera na uadilifu.
“Hili ni zoezi la kikatiba na msingi wa kukuza demokrasia. Ni fursa ya wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka. Wito wangu kwa vyama vyote: shindaneni kwa hoja, si matusi wala uchochezi,” ameongeza.
Katika kuhitimisha, Rais Samia ametoa wito mahsusi kwa vyama vya siasa kuhakikisha wanatoa nafasi za kutosha kwa wanawake na vijana katika kugombea nafasi mbalimbali, akisema huo ndio msingi wa kujenga taifa jumuishi.
“Nitumie fursa hii kuhimiza vyama vyote vya siasa kuwapa nafasi wanawake na vijana. Taifa letu linawahitaji,” amesema Rais Samia.
Imeandaliwa na Mwandishi Wetu



