Waandishi wa habari watakiwa kujiunga NSSF

DAR ES SALAAM: Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, aliyewakilishwa na Dk James Kalanje, amewataka waandishi wa habari na wafanyakazi wa sekta ya habari kujiunga na Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Hiari (Hifadhi Scheme) wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kujijengea usalama wa kipato na huduma za afya kwa siku zijazo.

Kalanje ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina maalumu ya kuhamasisha wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kujiunga na mfumo huo, ulioandaliwa na NSSF.

Amesema waandishi wa habari ni mhimili muhimu wa maendeleo ya taifa, lakini wengi wao, hususan wanaojitegemea na wanaofanya kazi katika sekta binafsi, bado hawapo katika mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii, hali inayowaweka katika mazingira magumu wanapostaafu, kuugua au kupoteza uwezo wa kufanya kazi.

Kalanje amesema takwimu zisizo rasmi zinaonesha zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawako katika mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii, akisisitiza kuwa Hifadhi Scheme ni fursa muhimu kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na waliojiajiri kuweka akiba kulingana na uwezo wao na kujihakikishia kipato cha uzeeni pamoja na huduma za bima ya afya.

Aidha, amewataka wanahabari kutumia taaluma yao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, huku akiwataka waajiri wa vyombo vya habari kuweka mazingira yatakayowahamasisha wafanyakazi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NSSF Kinondoni, Gerald Mkonyi, amewataka waandishi wa habari kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba mapema kupitia Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Hiari (Hifadhi Scheme), akisema hatua hiyo itawasaidia kuwa na uhakika wa kipato na ustawi wanapofikia umri wa uzee.

Naye Mwenyekiti wa (JOWUTA), Mussa Juma, ameipongeza NSSF kwa kuendelea kuwafikia waandishi wa habari na makundi mengine yaliyo katika sekta isiyo rasmi, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa wananchi na ushiriki wao katika mifumo ya hifadhi ya jamii.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya, amesema chama hicho kina jumla ya wanachama 500, kati yao 150 wakiwa wanatoka Mkoa wa Dar es Salaam.

Ameomba NSSF kuendelea kufikisha elimu hiyo kwa wanachama waliopo mikoani ili nao wanufaike na fursa zinazotolewa kupitia Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Hiari.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button