Wakazi Nanda kunufaika na mradi wa shule

WAKAZI wa kjiji cha Nanda kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara watanufaika na mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya Nanda uliyogharimu zaidi ya Sh milioni 500.
Akielezea faida watakazozipata wakazi hao katika ujenzi wa mradi huo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Abina Saidi amesema mradi huo umewaondolea adha wanafunzi kufata elimu vijiji jirani.
“Kabla ya ujenzi huu watoto walikuwa wakitembea umbali kutoka hapa kijijini kwenda vijiji vya jirani kufata elimu ya sekondari kama vile mpotola,” amesema Saidi.
Mradi huo licha ya kunufaisha wakazi wa kijiji hicho, lakini pia vijiji vingine kama vile kijiji cha Mmovo, Mnali, Namkonda na vijingine.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Friday Sondasy amesema shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 150, ujenzi ambao umepunguza mlundikano wa wanafunzi katika shule ya sekondari mpotola iliyopo kwenye halmashauri hiyo.
Pia kuwapunguzia umbali wa kilometa kilomita sita walizokuwa wakitembea kutoka kijiji hicho cha Nanda kwenda sekondari hiyo ya mpotola kwenye halmashauri hiyo.
Baadhi ya wazazi kijijini hapo, akiwemo Hassan Halidi “Tunaishukuru sana serikali yetu ya awamu ya sita kutujengea hii shule na kutuondolea adha ya watoto kutembea umbali mrefu kufata shule”
Baadhi ya wanafunzi shuleni hapo akiwemo Shadraki Ayubu kutoka kidato cha kwanza ameishukuru serikali kuwaletea ujenzi wa shule hiyo kwenye kijiji chao kwa sababu umewarahisishia upatikanaji wa elimu.
Shaloni Saidi mwanafunzi wa kidato hicho” Kabla ya huu mradi tulikuwa tunapitia changamoto ya kutembea kutoka hapa kwenda vijiji jirani kufata masomo ila sasa hivi tunaishukuru kwa kutujengea shule na tunaahidi kusoma kwa bidii ili tufaulu mzuri”
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amezindua ujenzi wa mradi huo na kuahidi kutoa komputa 10 pamoja na masuala mengine kwa ajili ya kuendelea kuboresha upatikanaji wa elimu shuleni hapo, kupata elimu kwa utulivu kisha wajipatie maendeleo.
Aidha Waziri huyo ameendelea na ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani humo kwa ajili ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoianza Oktoba 6, 2024.