Wanafunzi, wazazi wanufaika na ushauri wa elimu kimataifa

MWANZA: WAZAZI, walezi na wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini wameanza kupata mwanga zaidi kuhusu fursa za elimu ya juu nje ya nchi kupitia maonesho ya Global Education Fair 2026 yanayoandaliwa na Global Education Link (GEL).

Maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa jamii kupata taarifa sahihi kuhusu uchaguzi wa kozi, vyuo vikuu, nafasi za ufadhili wa masomo (scholarships), gharama za masomo pamoja na taratibu za kupata visa na maandalizi ya maisha ya mwanafunzi anayeenda kusoma nje ya nchi.

Kwa mujibu wa GEL, jumla ya watu 1,113 wakiwemo wanafunzi, wazazi na walezi wamefikiwa kupitia maonesho yaliyofanyika Zanzibar, Dodoma na Dar es Salaam, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuwafikia wakazi wa Kanda ya Ziwa kupitia maonesho yatakayofanyika jijini Mwanza Julai 30, 2026.

Mkurugenzi Mtendaji wa GEL, Abdulmalik Mollel, alisema mwitikio wa jamii unaonesha kuwa kuna uhitaji mkubwa wa mwongozo sahihi kwa wanafunzi wanaotaka kuendelea na elimu ya juu.

Alisema maonesho hayo yanasaidia kupunguza changamoto ambazo wanafunzi wengi hukutana nazo wakati wa kufanya maamuzi ya taaluma, hasa kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu vyuo na fursa zilizopo.

“Tunataka mwanafunzi afanye maamuzi sahihi kuhusu kozi na chuo kulingana na uwezo wake, malengo yake na mahitaji ya soko la ajira, badala ya kufuata mkumbo,” alisema Mollel.

Kupitia maonesho hayo, wanafunzi wamepata nafasi ya kukutana moja kwa moja na wawakilishi wa vyuo mbalimbali vya kimataifa na kupata ushauri unaozingatia matokeo yao ya kitaaluma pamoja na uwezo wao wa kifedha.

Mbali na kuwasaidia kupata udahili, GEL imeeleza kuwa inalenga kuwawezesha vijana kuchagua taaluma zenye mchango katika maendeleo ya taifa, ikiwemo sayansi za afya, teknolojia, uhandisi, akili bandia, sayansi ya data, nishati, kilimo cha kisasa na biashara.

Kwa upande wa jamii ya Mwanza na mikoa jirani, maonesho hayo yanatarajiwa kuwa fursa kwa wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne, Kidato cha Sita, stashahada, shahada na wanaotafuta masomo ya uzamili kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa elimu.

GEL imewataka wanafunzi wanaotarajia kushiriki kufika na vyeti au matokeo yao ili kupata mwongozo unaoendana na uwezo na malengo yao ya kielimu.

Maonesho hayo yanaendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na jamii katika kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi na kutumia elimu kama nyenzo ya kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button