Watanzania wapata nafasi mpya TPSC

DAR ES SALAAM: Watanzania wanaotaka kuongeza elimu na kujenga taaluma wamepata fursa mpya baada ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuanzisha programu mpya za shahada katika Kampasi za Tabora na Dar es Salaam kwa Mwaka wa Masomo 2026/2027.
Fursa hizo zinatarajiwa kuwawezesha wanafunzi na watumishi kujiendeleza katika taaluma mbalimbali zinazohusiana na usimamizi wa rasilimali watu, kumbukumbu na taarifa pamoja na uhazili na utawala.
Mkuu wa TPSC, Dk Ernest Mabonesho, amesema kuanzishwa kwa programu hizo ni sehemu ya jitihada za chuo hicho kupanua fursa za elimu ya juu kwa Watanzania na kuwaandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya Utumishi wa Umma na taasisi mbalimbali nchini.
“Kuanzishwa kwa programu hizi za Shahada ni hatua muhimu katika juhudi za TPSC za kupanua fursa za elimu ya juu kwa Watanzania. Tunataka kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fursa ya kujenga taaluma katika maeneo ambayo ni muhimu kwa ufanisi wa taasisi na maendeleo ya Utumishi wa Umma,” amesema Dk Mabonesho.
Amefafanua kuwa Kampasi ya Tabora imeanza kutoa Shahada ya Usimamizi wa Kumbukumbu, Nyaraka na Taarifa (Bachelor Degree in Records, Archives and Information Management) pamoja na Shahada ya Uhazili na Utawala (Bachelor Degree in Secretarial Duties and Administration).
Kwa upande wa Kampasi ya Dar es Salaam, TPSC imeongeza Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (Bachelor Degree in Human Resource Management), inayolenga kuandaa wataalamu katika eneo la usimamizi wa rasilimali watu kwa taasisi za umma na binafsi.
Dk Mabonesho amesema programu hizo zitatoa nafasi kwa wanafunzi na watumishi wanaotaka kuendeleza elimu yao katika fani hizo, huku zikiendana na mabadiliko ya mazingira ya kazi na mahitaji ya soko la ajira.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya TPSC ya kutoa elimu na mafunzo yanayokidhi mahitaji ya kitaaluma na kiutendaji, sambamba na kuongeza uwezo wa wataalamu watakaoshiriki katika utoaji wa huduma na maendeleo ya taasisi mbalimbali nchini.



