SHIRIKA la World Vision Tanzania limeliomba bunge kuishauri serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya ulinzi wa watoto katika kupambana na vitendo vya kikatili ikiwamo mimba na ndoa za utotoni.
Akizungumza jijini hapa, Mwenyekiti wa Bodi Shirika la World Vision Tanzania, Dk Diana Mndeme alisema ni vyema bunge likashauri serikali kuongeza bajeti ya ulinzi wa watoto ikiwa ni njia ya kupambana na vitendo vya ukatili.
Alisema shirika pia limeliomba bunge kuendelea kufanyia kazi suala la mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hasa katika kifungu cha 13 (1) na kifungu cha 17.
Aidha, Shirika la World Vision Tanzania limetoa mapendekezo kwa serikali kama mtekelezaji wa sheria na mambo mengine muhimu kwa ustawi wa mtoto ikiwamo kufanya mashindano kama hayo katika maeneo mengine ambako shirika halijafika.
Pia ameiomba serikali kuanzisha huduma ya mkono kwa mkono katika kila mkoa na kila wilaya ili kuweza kuwahudumia waathirika wa ukatili kwa urahisi zaidi.
Alisema serikali iendelee kusimamia sheria na kuchukua hatua stahiki kwa wanaohusika katika kusababisha mimba, ndoa za utotoni na ukatili wowote dhidi ya watoto.
Pia aliomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto kuharakisha uanzishwaji au uundwaji wa madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto shuleni na uanzishwaji wa mfumo mpya wa uundaji wa mabaraza ya watoto.