Wanaume watahadharishwa afya ya matiti

DAR ES SALAAM: WANAUME wametakiwa kuwa makini na afya ya matiti na kutopuuza mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida katika eneo hilo, ikiwemo kuonekana kwa uvimbe, kwa kuwa saratani ya matiti inaweza pia kuwapata wanaume.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Daktari Bingwa wa Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Emmanuel Nundu, wakati akitoa elimu kuhusu saratani ya matiti kwa wanaume kwa wanachama wa Rotary Club Dar es Salaam.

Dk. Nundu amesema mwanaume anapobaini mabadiliko yasiyo ya kawaida katika matiti, ni muhimu kufika katika kituo cha afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata ushauri wa kitaalamu, badala ya kuyapuuza au kusubiri hali hiyo kuendelea.

Amesema jamii inapaswa kuondokana na dhana kwamba saratani ya matiti ni ugonjwa unaowahusu wanawake pekee, kwa kuwa wanaume nao wanaweza kuugua saratani hiyo, hivyo elimu na uelewa kuhusu viashiria vyake ni muhimu.

“Ni muhimu kuongeza uelewa kuhusu saratani ya matiti kwa wanaume, ili jamii iweze kutambua mabadiliko yasiyo ya kawaida na kuchukua hatua stahiki kwa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na ushauri wa wataalamu,” amesema Dk. Nundu.

Akizungumzia huduma zinazotolewa na ORCI, Dk. Nundu amesema taasisi hiyo ina wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika vifaa na teknolojia za kisasa zinazolenga kuimarisha huduma na kuongeza fursa kwa wagonjwa kupata huduma stahiki kwa wakati.

“Uwepo wa mashine za kisasa za tiba ya mionzi pamoja na vifaa vingine vya uchunguzi na matibabu ya saratani ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuboresha huduma za saratani nchini,” amesema.

Dk. Nundu amesema pamoja na uwekezaji katika vifaa na teknolojia, elimu kwa jamii ina nafasi muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya saratani kwa kuwasaidia watu kuwa na uelewa wa mabadiliko yanayopaswa kupewa umakini na wakati wa kutafuta huduma za kitaalamu.

Kwa upande wake, Rais wa Rotary Club Dar es Salaam, Lenah Munyua, ameishukuru ORCI kwa kuwapatia wanachama wa klabu hiyo elimu kuhusu saratani ya matiti kwa wanaume, akisema elimu hiyo imewasaidia kupata uelewa ambao hapo awali hawakuwa nao kuhusu uwezekano wa wanaume kuugua saratani hiyo.

Lenah amesema elimu hiyo imewafungua macho na kuwasaidia kuelewa kuwa wanaume pia wanahitaji kuwa makini na afya zao, ikiwemo kufuatilia mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida katika matiti na kutafuta ushauri wa wataalamu wa afya wanapohitaji.

Amesema Rotary Club Dar es Salaam iko tayari kushirikiana katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa saratani na kuchukua hatua mapema pale mtu anapobaini mabadiliko yanayoweza kuashiria tatizo la kiafya.

Amesema Rotary Club itaendelea kuwa sehemu ya juhudi za kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kulinda afya, ikiwa ni pamoja na kuwahimiza watu kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na kupata matibabu mapema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button