MOI yaja na teknolojia mpya kutibu kiharusi

DAR ES SALAAM: Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza kutumia teknolojia ya kisasa kutoa matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo kwa wagonjwa wa kiharusi inayongeza ufanisi wa matibabu.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Ubongo MOI, Dk Lemeri Mchome, amesema teknolojia hiyo ni ya kwanza kutumika nchini na kwamba inakwenda kuleta mapinduzi katika matibabu ya ugonjwa huo.
“Tunatoboa tundu ndogo kichwani na tunapitisha kifaa maalumu chenye kamera, Ile kamera inakwenda kutuonyesha eneo ambalo damu imevilia na kutuwezesha kuitoa bila kuathiri sehemu nyingine,”
“Hii ndiyo teknolojia ya kisasa zaidi duniani na sisi kama taasisi hatuko nyuma, wagonjwa wa kiharusi hawana sababu ya kukimbilia nje ya nchi kwa matibabu, huduma hiyo inapatikana MOI,” amesema Dk Lemeri.

Naye, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo MOI, Dk John Mtei, ambaye ameshiriki katika upasuaji wa kwanza kwa kutumia kifaa hicho amesema technolojia hiyo inaacha alama katika mapinduzi ya tiba ya Kiharusi nchini.
“Ufanisi wa matibabu ndiyo nyenzo muhimu katika matumizi ya technolojia hii, mgonjwa anafanyiwa upasuaji na kuondolewa tatizo lake kwa uhakika,” amesema Dk Mtei.



