Waziri Kairuki atoa maagizo utekelezaji mradi FTTH

DODOMA; WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ameliagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa Fiber to the Home (FTTH), ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma ya intaneti kupitia mkongo wa taifa.

Kairuki ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Amesema mafanikio ambayo TTCL imeanza kuyapata kwa kurejea kupata faida na kulipa gawio kwa serikali yanapaswa kuendana na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Amebainisha kuwa Mkoa wa Dodoma umepewa lengo la kufikisha maunganisho 32,000 ya FTTH ifikapo Agosti mwaka huu na kuwataka watendaji wa TTCL kuongeza juhudi ili kufikia lengo hilo.

Kwa mujibu wa Kairuki, Wilaya ya Mpwapwa bado ina idadi ndogo ya watumiaji wa huduma hiyo, ambapo wateja 60 waliopo hawakidhi mahitaji yaliyopo, huku mkoa ukiwa na zaidi ya wateja 63,000 wa huduma mbalimbali za TTCL.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlembule, alisema Serikali inaendelea kuboresha huduma za mawasiliano kupitia ujenzi wa minara 636 unaotarajiwa kukamilika Machi mwaka ujao, sambamba na mradi mwingine wa minara 280 unaoendelea nchini.

Amesema tathmini ya Serikali imebaini maeneo 290 yenye changamoto za mawasiliano, huku Wilaya ya Mpwapwa ikiwa na maeneo tisa yanayohitaji kuboreshwa huduma hizo. Aliongeza kuwa wilaya hiyo tayari ina minara 57 iliyowezesha huduma kufika katika kata 28, huku kata tano zikiwa bado hazijafikiwa.

Kairuki alisema Serikali pia itajenga minara mipya katika Kata za Ipera, Mhasa, Chunyu, Godegode, Gulwe, Kimagai na Kiboriani, akisisitiza kuwa mawasiliano ni huduma muhimu kwa sekta za afya, elimu, biashara na uchumi wa kidijitali.

Awali, Meneja wa Kanda wa TTCL, Saimon Marwa, alisema wananchi wanaweza kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa huduma ya FTTH katika ofisi za TTCL bila kulipia gharama za kuunganishiwa, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya intaneti katika kaya nyingi zaidi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button