Shirika la Camara lazindua kituo cha kidijitali shule ya umma Nyasa

NYASA, RUVUMA: Shirika la Camara Education Tanzania limezindua rasmi kituo cha kidijitali cha kujifunzia katika Shule ya Sekondari Mkali iliyoko wilayani Nyasa, mkoa wa Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Nasoma, unaolenga kuongeza upatikanaji wa elimu inayotumia teknolojia katika shule za umma nchini Tanzania.
Mradi wa Nasoma unatekelezwa na Camara Education Tanzania kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI,) kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi na walimu kutumia TEHAMA na rasilimali za kidijitali katika ufundishaji na ujifunzaji.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024, Mradi wa Nasoma umefikia jumla ya shule 35 katika Tanzania Bara na Zanzibar.
Uzinduzi wa kituo hicho umefanywa na Mbunge wa Jimbo la Nyasa, John Nchimbi, ambaye aliongoza hafla hiyo, ikiashiria kuanza rasmi matumizi ya kituo hicho kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi na walimu kupata fursa zaidi za kujifunza na kutumia teknolojia katika elimu.
Kituo hiki kina kompyuta za mezani 26, projector, TV janja, ‘whiteboard’, vifaa vya matengenezo ya TEHAMA, miundombinu ya mtandao wa ndani (LAN), pamoja na huduma ya intaneti.
Pia, kituo kina server yenye maudhui ya elimu yanayopatikana bila intaneti, kuwawezesha wanafunzi na walimu kupata rasilimali za kujifunzia hata katika mazingira yenye changamoto za upatikanaji wa intaneti.
Kupitia kituo hiki, wanafunzi watapata fursa ya kujenga ujuzi wa kidijitali, kufanya tafiti, kupata rasilimali za kielimu na kutumia teknolojia kama sehemu ya uzoefu wao wa kila siku wa kujifunza. Walimu pia watanufaika kwa kupata mazingira yanayowawezesha kutumia zana za TEHAMA katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuendeleza ujuzi wao wa kitaaluma.
Mradi huu wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 35, unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka minne, ambapo Camara Education Tanzania itaendelea kutoa usimamizi wa karibu, ufuatiliaji na usaidizi wa kiufundi ili kuhakikisha kituo kinatumika ipasavyo na kinakuwa endelevu. Baada ya kipindi cha utekelezaji, umiliki wa Kituo hiki cha Kujifunzia Kidijitali utakabidhiwa kwa shule.
Uanzishwaji wa kituo hiki ni hatua nyingine ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuunganisha shule na fursa za kidijitali, na kuhakikisha wanafunzi wanapata zana, maarifa na mazingira yanayowawezesha kujifunza, kubuni na kujiandaa kwa ulimwengu unaozidi kutegemea teknolojia.
Mradi wa Nasoma Mradi wa Nasoma unatekelezwa na Camara Education Tanzania kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ukiwa na lengo la kuimarisha upatikanaji na matumizi ya teknolojia katika elimu kupitia uanzishwaji wa Vituo vya Kujifunzia Kidijitali katika shule za umma.
Camara Education Tanzania Camara Education Tanzania ni taasisi isiyo ya kiserikali inayolenga kuboresha elimu kupitia matumizi ya teknolojia kwa kuongeza upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA, maudhui ya kidijitali, mafunzo kwa walimu, pamoja na usaidizi wa kiufundi kwa shule na jamii.



