JNIA, KIA zang’ara tuzo za ACI AFRICA Nigeria

ABUJA: VIWANJA vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) vimeipa Tanzania heshima katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika baada ya kutwaa tuzo tatu zinazotolewa na Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika (ACI Africa).
Katika tuzo hizo, JNIA imetwaa tuzo mbili, ikiwemo nafasi ya pili katika kipengele cha Utawala Bora upande wa Uwezeshaji na Utayari wa Huduma kwa Abiria 2026 (Runner-Up of Passenger Facilitation and Readiness Excellence Awards 2026 – Governance Category).
JNIA pia imepata nafasi ya pili katika kipengele cha Ubunifu na Mageuzi ya Kiteknolojia (Innovation & Transformation Category) katika kundi la viwanja vya ndege vinavyohudumia kati ya abiria milioni mbili na milioni tano kwa mwaka.
Kwa upande wake, KIA imeibuka mshindi wa kwanza katika Tuzo ya Uwezeshaji na Utayari wa Huduma kwa Abiria 2026, katika kipengele cha Ushirikishwaji wa Wadau (Stakeholder Engagement), kwa kundi la viwanja vya ndege vinavyohudumia chini ya abiria milioni mbili kwa mwaka.
Tuzo hizo zimepokelewa na Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mzee Kilele, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo, katika hafla iliyofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 35 wa ACI Africa unaoendelea jijini Abuja.
Mkutano huo umeanza Septemba 19 na unatarajiwa kufungwa Septemba 25, 2026, ukiwa na kaulimbiu “Next-Gen Airports: Driving Performance and Resilience”, inayolenga kujadili namna ya kuimarisha utendaji, ubunifu, matumizi ya teknolojia na ustahimilivu wa viwanja vya ndege barani Afrika.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo, Mzee Kilele, amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa juhudi zinazofanywa na TAA katika kuboresha huduma, kuimarisha ushirikiano na wadau na kuweka mazingira bora ya kukuza shughuli za kibiashara na kiutendaji katika viwanja vya ndege nchini.
“Tuzo hizi ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na TAA kwa kushirikiana na wadau. Tunatambua kuwa ukuaji wa viwanja vya ndege unaenda sambamba na ubora wa huduma, ubunifu na uwezo wa kujenga mahusiano imara na wadau. Utambuzi huu unatupa nguvu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii, kuongeza ubunifu na kuhakikisha tunapata matokeo yanayoonekana,” amesema Kilele.

Ameongeza kuwa TAA itaendelea kutumia fursa mbalimbali za kibiashara na ubunifu katika sekta ya usafiri wa anga ili kuongeza ushindani wa viwanja vya ndege vya Tanzania na kuvifanya kuwa vituo vinavyokidhi mahitaji ya abiria, mashirika ya ndege na wadau wengine wa sekta hiyo.
Mafanikio ya JNIA na KIA yanaongeza mwonekano wa Tanzania katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kuboresha miundombinu, huduma na mazingira ya biashara katika viwanja vya ndege nchini.




