Norway, Tanzania zaandaa mfumo wa kufuatilia biashara ya kaboni

DODOMA: Serikali za Norway na Tanzania zimeshirikiana kuandaa mfumo wa kitaifa wa ukusanyaji ua uwekaji kumbukumbu taarifa za kaboni kwa lengo kuiwezesha nchi kufanya usimamizi rasilimali hiyo kwa uwazi.
Hayo yalibainishwa jijini Dodoma leo, Jumatano (Novemba 25, 2026), na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Hewa Ukaa (NCMC), Risper Koyi wakati wa kilele cha Kilele cha Wiki ya Tabianchi 2026 huku akisema kuwa mfumo huo utakaorekodi kiwango cha kaboni kinachozalishwa, kuuzwa na kuhamishwa nchini ili kuongeza uwazi, usimamizi na uaminifu katika biashara hiyo.
Koyi alisema mfumo huo wa kumbukumbu umeandaliwa kwa ushirikiano na ufadhili wa Serikali za Tanzania na Norway, ukiwa na lengo la kuweka taarifa sahihi za viwango vya kaboni inayozalishwa kupitia miradi mbalimbali.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kuanzishwa kwa mfumo huo kutaiwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za biashara ya kaboni, kufuatilia shughuli zinazotekelezwa nchini na kuhakikisha usimamizi wake unakuwa na uwazi.
“Ili kuwa na usimamizi wenye tija kituo kinarekodi takwimu za kaboni inayozalishwa nchini na kuuzwa ili kupata taarifa kamili na hatimaye kutambua namna gani biashara hii itachangia pato la taifa,” alisema Koyi.
Alisema NCMC imejikita katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kitaasisi ili kuwezesha maendeleo ya soko la kaboni, ikiwemo mifumo ya usajili, mipango, ufadhili na kuunganisha miradi ya ndani na wawekezaji wa kimataifa.
Aliongeza kuwa biashara ya kaboni ina mchango katika maendeleo ya taifa kwa kufungua fursa za uwekezaji, kuongeza mapato na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
SOMA: NCMC yavutia uwekezaji biashara ya kaboni
Alisema Tanzania inalenga kutumia fursa hizo kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikithamini mchango wa Serikali ya Norway katika kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mifumo ya hali ya hewa.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Maduhu Kazi alitoa wito kwa taasisi zilizohudhuria mkutano huo kushirikisha tafiti zao ili kuboresha dhima ya ushirikiano wa Tanzania na Norway katika utunzaji mazingira.
Alisema taasisi za kitafiti zina mchango mkubwa kuleta mawazo yatakayoboresha sera na hatimaye kufanikiwa kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mshauri Mwandamizi katika Wizara ya Mambo ya Nje wa ubalozi wa Norway nchini, Sondre Bjotveit alisema nchi hiyo ya Ukanda wa Scandinavia itaendelea kushirikiana na Tanzania kuleta suluhu ya mabadiliko ya tabianchi ili familia za Watanzania ziendelee kunufaika na rasilimali zitokanazo na mazingira yanayowazunguka.
Alisema licha ya mabadiliko yanaoonekana katika hali ya hewa, kukiwa na rasilimali fedha madhubuti na taasisi imara zitazoingia mstari wa mbele kufanya tafiti zitasaidia kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia biashara ya kaboni.



