Bil 19/-zalipwa fidia wakazi Arusha

ARUSHA: Serikali imetoa Sh bilioni 19 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa barabara za maandalizi ya AFCON 2027 jijini Arusha.

Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuanza malipo hayo mara moja ili kuwawezesha wananchi kupata stahiki zao na kuruhusu ujenzi kuendelea bila vikwazo.

Kadogosa ametoa maelekezo hayo wakati akikagua maendeleo ya miradi ya barabara za AFCON jijini Arusha, akisema fedha za fidia tayari zimetolewa na Serikali hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha malipo kwa wananchi wanaostahili.

Amesema malipo hayo yanapaswa kuanza ndani ya siku mbili hadi tatu ili wakandarasi waendelee na kazi bila kusimama.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali si kujenga barabara kwa ajili ya mashindano ya AFCON pekee, bali kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na miundombinu hiyo hata baada ya mashindano kumalizika.

“Tunataka kuona barabara hizi zinazojengwa kwa maandalizi ya AFCON 2027 zikiwa na ubora unaostahili na kuendelea kuwanufaisha wananchi hata baada ya mashindano hayo kumalizika,” amesema Kadogosa.

Katika ukaguzi huo, Kadogosa ameridhishwa na maandalizi ya wakandarasi katika utekelezaji wa miradi hiyo na kupongeza TANROADS kupitia Kitengo cha TECU kwa usimamizi wa mradi.

Aidha, amemtaka mkandarasi kuongeza vifaa, mitambo na nguvu kazi katika maeneo yote ya ujenzi ili kuongeza kasi ya kazi kwa kufanya kazi saa 24, mchana na usiku, na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amesema wakandarasi wamekamilisha kwa asilimia 100 uhamishaji wa vifaa na mitambo katika maeneo ya miradi pamoja na kuweka wataalamu wanaohitajika.

Amesema hatua hiyo imechangia kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, ambazo zinaendelea kufanyika mchana na usiku.

Naye, Msimamizi wa Mradi wa Barabara ya Mbauda–Losinyai yenye urefu wa kilometa 70 kutoka TECU, Mhandisi Hophine Mollel, amesema kipande cha kilometa 13 kinachotekelezwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 kimefikia asilimia 54.4 ya utekelezaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button