Wananchi wanufaika msaada wa kisheria

ARUSHA: WANANCHI 11,715 wamefikiwa kupitia kliniki za msaada wa kisheria zilizoanzishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mikoa tisa nchini, kwa lengo la kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, kutatua migogoro na kupunguza mashauri yasiyo ya lazima mahakamani.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kamati za ushauri wa kisheria na kliniki za msaada wa kisheria mkoani Arusha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, alisema kliniki hizo zinazotolewa bila malipo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanasikilizwa na kero zao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amesema huduma hizo zimeanza kutolewa Arusha kuanzia Novemba 24 hadi 29, 2026, katika Viwanja vya Sanawari, huku mikoa mingine iliyofikiwa ikiwa ni Kilimanjaro, Mwanza, Singida, Manyara, Simiyu, Dar es Salaam, Tanga, Katavi na Dodoma.

Amesema kupitia kliniki hizo, mawakili wa serikali na wa kujitegemea wanatoa ushauri wa kisheria bure, hatua inayolenga kuimarisha usuluhishi, utawala wa sheria na kupunguza hasara zinazoweza kutokana na migogoro ya kisheria kwa wananchi na serikali.

Aidha, aliahidi kusikiliza malalamiko ya wananchi, ikiwemo mgogoro wa soko la Kwa Sadala mkoani Kilimanjaro ili wafanyabiashara waweze kurejea na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

Naye Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, amesema serikali imetafsiri sheria zaidi ya 446 kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao, huku Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, George Mandepo, akieleza kuwa mifumo 28 ya sheria inatarajiwa kufanyiwa mapitio na maboresho katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili iendane na mahitaji ya sasa na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button