Mgongolwa asifu utendaji jeshi la Polisi Iringa

IRINGA: Juhudi za kuimarisha nidhamu, weledi na ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi zimetajwa kuwa miongoni mwa hatua zinazochangia kupunguza uhalifu na kurejesha imani ya wananchi kwa chombo hicho cha ulinzi na usalama mkoani Iringa.

Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Hamasa, Vijana na Michezo ya Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Joseph Mgongolwa, amesema mabadiliko yanayoonekana katika utendaji wa Jeshi la Polisi mkoani humo yanadhihirisha umuhimu wa uongozi wenye usimamizi madhubuti, nidhamu na kujituma katika kutekeleza majukumu ya kulinda raia na mali zao.

Amesema chini ya uongozi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Allan Mukumbi, kumekuwa na juhudi za kurejesha heshima ya jeshi hilo, kuboresha utendaji wa askari na kuimarisha mahusiano kati ya polisi na wananchi.

Mgongolwa amesema moja ya mabadiliko yanayostahili kupongezwa ni kuimarika kwa dhana ya Polisi Jamii, ambayo imewafanya wananchi kuondokana na hofu na kuanza kushirikiana na askari kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na viashiria vyake.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa sababu mapambano dhidi ya uhalifu hayawezi kuachiwa Jeshi la Polisi pekee, bali yanahitaji wananchi kuwa sehemu ya ulinzi na usalama wa maeneo wanayoishi.

“Leo tunaona wananchi wanashirikiana na Jeshi la Polisi kwa uwazi zaidi, wanatoa taarifa na kusaidia kubaini wahalifu. Hili ni jambo kubwa kwa sababu usalama wa wananchi hauwezi kupatikana bila ushirikiano wao na vyombo vya dola,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi za kamanda huyo hazijaishia katika usimamizi wa askari pekee, bali pia amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali na kuimarisha mazingira ya kazi kwa kuboresha vitendea kazi, ikiwamo kufufua magari ya polisi yaliyokuwa yameharibika na kuyarejesha katika matumizi.

Amesema hatua hiyo imeongeza uwezo wa vituo vya polisi kutoa huduma kwa wakati na kurahisisha askari kuwafikia wananchi wanapohitaji msaada wa kiusalama.

Pia, amepongeza ujenzi na uboreshaji wa vituo vya polisi pamoja na mwenendo wa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, akisema nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ni sehemu ya mabadiliko yanayoonekana mkoani humo.

Kwa mujibu wa Mgongolwa, taarifa alizozieleza zinaonesha kuwa matukio ya uhalifu, yakiwamo mauaji na ubakaji, yamepungua kwa kiwango kikubwa.

Pongezi hizo zinakuja wakati Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akisisitiza umuhimu wa nidhamu, maadili na weledi ndani ya Jeshi la Polisi katika hotuba yake kwa viongozi na maofisa waandamizi wa jeshi hilo, kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maofisa hao, uliofanyika Novemba 20, mwaka huu, katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Rais Samia alisisitiza kuwa askari wanaokiuka maadili na taratibu za kazi wanapaswa kuwajibishwa, huku akilitaka jeshi hilo kuimarisha ushirikiano na wananchi na kutopuuza taarifa zinazohusu usalama.

Aidha, alihimiza kuendelezwa kwa elimu ya Polisi Jamii, ikiwamo kuwafikia watoto na vijana mashuleni na katika nyumba za ibada, ili kuwajengea misingi ya maadili, nidhamu na kuheshimu sheria tangu wakiwa wadogo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button