Serikali kujizatiti usimamizi bandari ya Mbamba Bay

RUVUMA: SERIKALI imesema itaendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuzingatia viwango vya kitaalamu ili kuimarisha biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Kusini na nchi jirani.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo Novemba 20, 2026, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo, ambao umefikia asilimia 78 ya utekelezaji.
Alisema Serikali imetenga Sh bilioni 75.8 kwa ajili ya mradi huo, ambao ukikamilika utawezesha bandari kuhudumia meli mbili zenye uzito wa tani 5,000 kila moja kwa wakati mmoja.

Alieleza kuwa kukamilika kwa bandari hiyo kutarahisisha usafirishaji wa mizigo kupitia Ziwa Nyasa, kuongeza ufanisi wa biashara na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Kusini na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia.
Profesa Mbarawa alisema Serikali pia inapokea na kufanyia kazi maombi ya wadau wa usafirishaji wanaotaka kuboreshwa kwa huduma za usafiri katika ukanda huo.
Alisema miongoni mwa maombi yanayofanyiwa tathmini ni kuongeza safari za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwenda Songea kutoka nne hadi tano kwa wiki, hatua itakayozingatia mahitaji ya soko.

Aidha, alisema Serikali inapokea ombi la kuongeza vyombo vya usafiri katika Ziwa Nyasa ili kuboresha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo.
Waziri Mbarawa alimtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi inazingatia usanifu na viwango vya kitaalamu vilivyoainishwa, akisisitiza kuwa miundombinu inayojengwa inapaswa kuwa imara na kudumu ili kulinda uwekezaji wa Serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, alisema kukamilika kwa bandari hiyo kutachochea shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kipato cha wananchi pamoja na kukuza mapato ya Serikali.
Alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na kufungua fursa za uwekezaji, biashara na maendeleo katika mkoa huo.

Aliongeza kuwa bandari hiyo inatarajiwa kuongeza nafasi ya Ruvuma katika biashara ya kikanda na kuchangia kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Kusini.
Awali, Meneja wa Mradi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), John Paul, alisema ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay unatarajiwa kukamilika Februari 26, 2027.
Alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 115, yadi ya kuhifadhi makasha 4,000, jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia watu 400 pamoja na maghala matatu ya kuhifadhi mizigo.
Alieleza kuwa miundombinu hiyo itakapokamilika itarahisisha usafirishaji wa madini, mazao ya kilimo na bidhaa za viwandani, huku ikiimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zinazopakana kupitia Ziwa Nyasa.



