Chumi kuongoza Bodi ya Ushauri YIA

IRINGA: MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Cosato Chumi, ameteuliwa kuongoza Bodi ya Ushauri ya Youth Investors Association (YIA), taasisi inayolenga kukuza uwekezaji, ujasiriamali na kuwawezesha vijana kiuchumi.
Katika nafasi hiyo, Chumi anatarajiwa kutumia uzoefu wake katika diplomasia, utumishi wa umma na uongozi kuishauri taasisi hiyo kuhusu namna ya kuimarisha mazingira yatakayowawezesha vijana kushiriki katika shughuli za uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.
Kupitia uteuzi huo, YIA inalenga kuimarisha nafasi ya vijana katika uchumi kwa kuwaunganisha na fursa za uwekezaji, kukuza ubunifu, kuwajengea uwezo wa ujasiriamali na kuongeza ushiriki wao katika mijadala na maamuzi yanayohusu maendeleo ya kiuchumi.
Chumi ana uzoefu wa uongozi na utumishi katika taasisi mbalimbali za umma. Kabla ya kujiunga na EALA, alihudumu kama Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kuanzia mwaka 2015 hadi 2025, akiwakilisha jimbo hilo kwa vipindi viwili vya uchaguzi.
Pia, aliwahi kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2024 hadi 2025. Vilevile, alikuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Uzoefu wake katika masuala ya diplomasia ulianza alipohudumu kama Afisa wa Diplomasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 2007 hadi 2015.
Awali, kati ya mwaka 2002 na 2006, alifanya kazi katika Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambako alipata uzoefu katika utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa maelezo ya YIA, Chumi ana dhamira ya kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia uwekezaji, ujasiriamali, mafunzo ya ujuzi na ubunifu.
Mtazamo huo unasisitiza umuhimu wa kuweka mifumo itakayowawezesha vijana kupata mitaji, maarifa na mitandao ya kibiashara, pamoja na kushiriki katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao.
Kupitia nafasi hiyo, anatarajiwa kuchangia katika kuimarisha juhudi za YIA za kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana na kuwawezesha kushiriki katika maendeleo ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.



