TTCL yatambuliwa kimataifa

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi kupitia upanuzi wa huduma za intaneti ya kasi, hatua inayolenga kuongeza fursa za biashara, ajira, elimu na huduma za kidijitali, sambamba na juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kujenga uchumi wa kidijitali nchini.

Juhudi hizo zimeendelea kulitangaza Tanzania kimataifa baada ya TTCL kutambuliwa kwa mara ya pili kutokana na mchango wake katika kuendeleza huduma za Fiber to the Home (FTTH), na kutunukiwa tuzo ya Gigacity Champion Award katika Kongamano la World Broadband Association (WBBA) Broadband Development Congress 2026 lililofanyika Novemba 16, jijini Cape Town, Afrika Kusini.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, ameeleza namna Shirika linavyowekeza katika miundombinu ya kisasa ya mawasiliano ili kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti zenye kasi na ubora nchini.

Katika wasilisho lake lenye mada “Unlocking the Broadband Innovation for Tanzania’s Digital Future”, Marwa ameeleza mikakati ya TTCL kupanua huduma za FTTH, kuimarisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) pamoja na kutumia teknolojia ya akili bandia (AI) kuboresha huduma na uzoefu wa wateja.

Aidha, amesema TTCL inalenga kufikisha huduma za FTTH katika maeneo mengi zaidi nchini kupitia mpango wa kuunganisha nyumba milioni moja ndani ya miaka mitatu, ambapo katika mwaka mmoja tayari miundombinu ya maunganisho takribani 300,000 imekamilika.

Utambuzi huo wa kimataifa unaongeza nguvu katika juhudi za Serikali za kutekeleza Dira ya Taifa ya Uchumi wa Kidijitali, kwa kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, kuvutia uwekezaji na kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi na wafanyabiashara kutumia teknolojia kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button