Madini ya Sh Bil 1.3 yakamatwa Dar yakitoroshwa

DAR ES SALAAM; Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanaojihusisha na utoroshaji wa madini, baada ya kukamatwa kwa dhahabu yenye uzito wa kilogramu 4.4 iliyokuwa ikisafirishwa kinyume cha sheria, yenye thamani ya Shi bilioni 1.38.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 27 Dar es Salaam, Mavunde amesema dhahabu hiyo ilikamatwa na vyombo vya dola katika eneo la Kiluvya, mkoani Dar es Salaam, Julai 25, 2026, ikiwa haikupitia mfumo rasmi wa biashara ya madini.
Amesema kitendo hicho kingesababisha serikali kupoteza mapato ya takribani Shilingi milioni 180.8 na kueleza kuwa kwa mujibu wa sheria, dhahabu hiyo imetaifishwa na kwa sasa ipo chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Amewataka wadau wote wa sekta ya madini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za biashara ya madini, akisisitiza kuwa utoroshaji wa madini unainyima serikali mapato ambayo yangetumika kuboresha huduma muhimu za kijamii kama elimu na afya.
Amesema serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini kupitia vituo 117 vya ununuzi wa madini na masoko 44 ya madini yaliyopo nchini, ili kuhakikisha madini yote yanauzwa kupitia mifumo rasmi.
Amesisitiza kuwa mtu yeyote atakayekutwa na madini bila kibali halali au bila kuyapitisha kwenye masoko rasmi atachukuliwa hatua za kisheria, madini hayo yataifishwa na kupelekwa BoT.

Amesema lengo la Serikali si kuwakamata wasafirishaji pekee, bali kuvunja mtandao mzima wa biashara haramu ya madini kwa kuwafikisha wote wanaohusika mbele ya vyombo vya sheria.
Vilevile, Mavunde amesema mtu yeyote atakayebainika kuhusika na utoroshaji wa madini na akiwa na leseni ya biashara ya madini, leseni yake itafutwa mara moja na atawekwa kwenye orodha ya watu wasiostahili kupata leseni tena (blacklist) ili asiruhusiwe kufanya shughuli yoyote ya madini nchini.



