TAEC yafanya ziara ukaguzi makasha

Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), ikiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Joseph Msambichaka, imefanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kujionea namna ukaguzi wa makasha kwa kutumia teknolojia ya skana unavyotekelezwa na jinsi TAEC inavyosimamia matumizi salama ya mionzi katika vifaa hivyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Msambichaka, amesema ameridhishwa na kiwango cha uzingatiaji wa usalama wa mionzi pamoja na ufanisi wa matumizi ya skana katika ukaguzi wa makasha bandarini.

“Tumekuja kujionea kazi inayofanywa na TAEC katika kusimamia matumizi salama ya mionzi kwenye skana zinazotumika bandarini. TAEC ndiyo yenye jukumu la kutoa leseni za matumizi ya vifaa hivi, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji wake. Tumejiridhisha kuwa mazingira ya kazi ni salama kwa wafanyakazi, madereva na wananchi kwa ujumla,” amesema Prof. Msambichaka.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia ya skana inayotumia mionzi katika ukaguzi wa makasha yameongeza ufanisi wa huduma bandarini kwa kupunguza muda wa ukaguzi, kuimarisha usalama wa biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Usalama wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Dk. Jumanne Fhika, amesema kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inatumia mashine 11 za skana ambazo zimeongeza ufanisi katika ukaguzi wa mizigo, kupunguza muda wa kuhudumia makasha na kuchangia ongezeko la mapato ya Serikali.

Katika kuendelea na ziara hiyo, wajumbe wa Bodi ya TAEC walitembelea pia eneo la ukaguzi wa mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), ambapo walijionea utekelezaji wa majukumu ya TAEC ya kusimamia na kudhibiti matumizi ya vifaa vya mionzi vinavyotumika kukagua mizigo inayoingia na kutoka nchini. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa wananchi, wafanyakazi na mazingira dhidi ya bidhaa au vifaa vinavyoweza kuwa na mionzi.

Aidha, Bodi ilitembelea Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Mionzi na Uchafuzi wa Anga kinachosimamia utekelezaji wa Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia (Comprehensive Nuclear-Test-Ban Treaty Organization – CTBTO).

Akitoa maelezo katika kituo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kimataifa kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia, ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizosaini na kuridhia mkataba huo.

Prof. Najat amesema kituo hicho kina jukumu muhimu la kufuatilia na kupima viashiria vya mionzi na uchafuzi wa anga, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa taifa, kulinda mazingira na kutekeleza wajibu wa Tanzania katika mfumo wa kimataifa wa ufuatiliaji wa majaribio ya nyuklia.

Ziara hiyo imeiwezesha Bodi ya TAEC kujionea kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Tume katika maeneo muhimu ya kimkakati, hususan usimamizi wa matumizi salama ya mionzi, ulinzi wa wananchi na mazingira, pamoja na mchango wa teknolojia ya nyuklia katika kuimarisha usalama na maendeleo ya uchumi wa nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button