Serikali yawaendeleza wabunifu 70

DAR ES SALAAM: Serikali imesema imefanikiwa kuwaendeleza wabunifu 70 waliotokana na mashindano ya Sayansi na Teknolojia (MAKSATU), huku ikiwa katika hatua za mwisho za kufanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ili iwe Sera ya Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Ujuzi, hatua inayolenga kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira na uchumi unaotegemea ubunifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu itakayofanyika kuanzia Agosti 15 hadi 24, 2026 katika Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wiki hiyo itajumuisha mashindano ya Sayansi na Teknolojia (MAKSATU), mashindano ya ujuzi, maonesho ya ubunifu pamoja na kongamano litakalojadili namna ya kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo, amesema Serikali inaendelea kukamilisha sera mpya ya Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Ujuzi, ambayo itaweka mazingira bora ya kukuza vipaji na ubunifu, sambamba na kuwawezesha wabunifu wanaochipukia kushindana katika soko la ndani na kimataifa.

Naye Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara hiyo, Profesa Ladislaus Mnyone, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu, wamesema Serikali imeanzisha madawati ya ubunifu katika halmashauri mbalimbali nchini ili kurahisisha wabunifu kuwasilisha mawazo yao, kupata ushauri na kuunganishwa na fursa za kuendeleza bunifu zao.




