Serikali yataka mikataba bora ya kazi

SERIKALI imevitaka vyama vya wafanyakazi nchini kuimarisha demokrasia ya ndani, kuongeza kasi ya kufunga mikataba ya hali bora za kazi na kuendeleza majadiliano ya kijamii ili kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija katika maeneo ya kazi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Dk. Eveline Munisi, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) unaofanyika mkoani Iringa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Dk. Munisi amesema demokrasia, uwazi na uwajibikaji ni misingi muhimu ya uongozi bora wa vyama vya wafanyakazi. Amesema viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kuwaunganisha wanachama na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba na sheria zinazosimamia vyama hivyo. “Demokrasia ndiyo nguzo kuu ya uendeshaji wa vyama vya wafanyakazi. Baada ya uchaguzi makundi yanapaswa kumalizika ili viongozi wapate nafasi ya kuwatumikia wanachama wote kwa umoja,” alisema.
Amewataka viongozi wa TUICO kusimamia kwa uwazi rasilimali za chama, kuimarisha mshikamano na kuhakikisha chama kinaendelea kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi. Dk. Munisi ameipongeza TUICO kwa kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995, akisema mafanikio yaliyopatikana yanaonyesha uimara wa chama hicho na mchango wake katika sekta ya ajira nchini.
Katika hatua nyingine, Serikali imeitaka TUICO kuongeza juhudi za kuhakikisha wafanyakazi wengi zaidi wananufaika na mikataba ya hali bora za kazi, ambayo ni nyenzo muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa wafanyakazi. “Naitaka TUICO kuongeza kasi ya kufunga mikataba ya hali bora za kazi inayokidhi mahitaji ya wafanyakazi katika mazingira ya sasa ya kazi,” alisema.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa majadiliano ya utatu kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi kwa kuwa ndiyo njia bora ya kujenga mahusiano mazuri kazini na kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo.Dk. Munisi amesema Serikali pia inaendelea kuboresha mazingira ya kazi yanayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuimarisha ujuzi wa wafanyakazi na kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi.
Amezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi pamoja na Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi ya mwaka 2025. SOMA: TUCTA yaahidi kutetea maslahi ya wafanyakazi
Aidha amewataka waajiri na wafanyakazi kuendelea kushirikiana katika kuongeza uzalishaji na ushindani katika maeneo ya kazi, akisisitiza kuwa pande hizo mbili ni washirika muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.”Waajiri si maadui wa wafanyakazi, bali ni wadau wao wakuu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa,” alisema.
Kuhusu haki za wafanyakazi, Dk. Munisi alisema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, huku Ofisi ya Kamishna wa Kazi ikiendelea kuchukua hatua dhidi ya waajiri watakaobainika kukiuka haki hizo. Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa TUICO, Abdallah Msese amesema katika kipindi cha miaka 30 iliyopita chama hicho kimeongeza idadi ya wanachama kutoka 32,000 hadi takribani 150,000.
Amesema pia chama kimepanua uwakilishi wake kutoka sekta mbili hadi nne na sasa kina ofisi katika mikoa 22 nchini. Msese amesema TUICO imeendelea kushiriki katika kufunga mikataba ya hali bora za kazi, kutatua migogoro ya kikazi na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi pamoja na waajiri. Amesema Mkutano Mkuu wa Saba unatarajiwa kutoa viongozi watakaosimamia juhudi za kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha mchango wa sekta ya kazi katika maendeleo ya Taifa.



