EAC yaongeza kasi ya ajenda ya biashara ya ndani

DAR ES SALAAM: Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa wito wa kuharakishwa kwa hatua za kuongeza biashara kati ya nchi wanachama, ikisema kiwango cha sasa hakijaendana na uwezo wa soko kubwa la kikanda

Akifungua Mkutano wa Wakuu wa Makampuni (CEOs Trade and Investment Roundtable) ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen Mbundi, amesema jumuiya hiyo imelenga kuongeza biashara ya ndani hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Amesema pamoja na hatua zilizopigwa kupitia Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Mfumo wa Forodha Moja, bado kuna changamoto zinazozuia wafanyabiashara kutumia kikamilifu fursa zilizopo.

Mbundi amesema biashara ya ndani ya EAC kwa sasa ni dola bilioni 19.7 za Marekani, ikilinganishwa na biashara na mataifa ya nje ya jumuiya yenye thamani ya dola bilioni 137, hali inayohitaji hatua zaidi za kukuza biashara ya kikanda.

“Ni muhimu kwa sekta binafsi kuwekeza katika bidhaa zenye ubora na ushindani badala ya kutegemea ulinzi wa masoko kupitia vikwazo vya biashara,”amesema.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Amedeus Mzee, amesema mapendekezo yatakayopatikana kwenye mkutano huo yatasaidia kuboresha sera za biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Gladness Salema, amesema mjadala wa ushirikiano wa kikanda unapaswa kuhamia katika kujenga uchumi wenye ushindani kupitia uzalishaji, ubunifu, teknolojia na minyororo ya thamani ya kikanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, Ahmed Farah, amesema biashara ya kikanda bado inakabiliwa na changamoto za kodi zisizotabirika, tofauti za viwango, taratibu ndefu za vibali, gharama kubwa za usafirishaji na vikwazo visivyo vya ushuru.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamiliki wa Viwanda Tanzania (CTI), Leodgar Tenga, amesema kuondoa changamoto hizo kutasaidia kuongeza uzalishaji wa viwanda na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Afrika Mashariki.

Mkurugenzi wa Nchi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Stephen Wambura, amesema upatikanaji wa fedha za muda mrefu ni muhimu katika kukuza uwekezaji wa viwanda, kilimo biashara na miundombinu.

Mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani, Maximilian Mueller, ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Afrika Mashariki na Ujerumani.

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo kujadili namna ya kuongeza biashara na uwekezaji ndani ya EAC.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button