TBS yatoa somo ubora wa bidhaa Kanda ya Magharibi

KIGOMA; Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi, limetoa wito kwa wazalishaji, wafanyabiashara pamoja na wananchi kutumia fursa za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, ili kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika soko Afrika Mashariki linalokuwa kwa kasi.
Akizungumza katika maonesho ya Lake Tanganyika Expo 2026 yaliyoanza Septemba 16 na yanatarajiwa kumalizika leo Septemba 22, 2026 Viwanja vya Community Center mkoani Kigoma, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Hamisi Seleleko alisema kuwa kanda hiyo inajumuisha mikoa mitatu ambayo ni Kigoma, Katavi, na Tabora.
Alisema kuwa lengo kuu la kushiriki katika maonesho hayo ni kutangaza huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS na kuwaonesha wajasiriamali na wazalishaji fursa zinazopatikana kupitia udhibitisho wa ubora wa bidhaa.
“Uthibitishaji wa ubora unampa mzalishaji fursa ya kuingiza bidhaa yake kwenye soko la ndani na nchi wanachama wa Afrika Mashariki, ambalo hadi sasa linajumuisha nchi nane,” alisema.

Aisema katika maonesho hayo, TBS imeweka dawati maalumu la kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi na wadau wanaotembelea banda lao na kutaja huduma hizo kuwa ni pamoja na usajili wa bidha,a kutoa elimu na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi.
Alisema usajili huo ni kigezo cha msingi kinachoonesha kuwa bidhaa hizo ni salama kwa matumizi ya jamii.
Pia alisema wanatoa elimu juu ya bidhaa zilizopigwa marufuku na kuwaonesha wananchi na wafanyabiashara mifano ya vipodozi na bidhaa zisizokidhi viwango au vyenye viambata hatari ambavyo vimepigwa marufuku, ili kuepuka madhara ya kiafya.
Aidha alitoa wito kwa wazalishaji wote kutumia fursa ya maonesho hayo kuwasilisha maombi yao kupitia mtandao na kukidhi vigezo ili maofisa wa TBS waweze kukagua maeneo yao ya uzalishaji, kupima bidhaa, na kuwapatia leseni ya kutumia alama ya ubora.



