Exim Bank yasogeza huduma za kifedha kwa madereva

DAR ES SALAAM: Madereva wa bodaboda, bajaji na magari wamepata fursa ya kufahamu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kulinda vyanzo vyao vya kipato kupitia ushiriki wa Benki ya Exim Tanzania katika tamasha la Twende BBM Festival 2026.
Benki hiyo iliyokuwa mdhamini wa tamasha hilo lililofanyika Novemba 14, 2026, ilitumia fursa hiyo kukutana na madereva wanaohusishwa na jukwaa la Twende na kuwafahamisha huduma zinazoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Jukwaa la Twende linahusisha madereva takribani 12,000 na jumuiya ya zaidi ya watumiaji 46,000 wa huduma zake.
Kupitia kampeni ya “Exim Inalinda Hustle Yako”, benki hiyo ilitambulisha huduma nne ambazo ni Exim Lipa ChapChap, Tumaini Health Insurance, Motor Insurance na Exim Quick Account, zinazolenga kurahisisha malipo, upatikanaji wa bima ya afya na ulinzi wa vyombo vya usafiri pamoja na huduma za kibenki.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo, alisema benki inatambua mchango wa madereva katika kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi, hivyo inaendelea kuwasogezea huduma zinazoweza kuwasaidia kusimamia shughuli zao na kulinda vipato vyao.
“Kwa madereva wengi, bodaboda, bajaji na magari si vyombo vya usafiri pekee, bali ni nyenzo muhimu za kujipatia kipato na kutunza familia zao. Tunatambua changamoto na mahitaji yanayoambatana na kazi zao za kila siku.

“Ndiyo maana kupitia huduma zetu, tunalenga kurahisisha upatikanaji wa malipo, kuwapatia fursa ya kupata ulinzi wa afya na vyombo vyao vya usafiri, pamoja na huduma za kibenki zinazowawezesha kusimamia fedha zao kwa urahisi zaidi. Hii ndiyo maana halisi ya ujumbe wetu, Exim Inalinda Hustle Yako,” alisema Lyimo.
Huduma ya Exim Lipa ChapChap inalenga kurahisisha upokeaji na ufanyaji wa malipo, huku Tumaini Health Insurance ikiwezesha madereva kupata ulinzi wa bima ya afya.

Kwa upande mwingine, Motor Insurance inatoa ulinzi wa bima kwa vyombo vya usafiri, wakati Exim Quick Account inawawezesha kufungua akaunti na kutumia huduma za kibenki za Exim.
Mmoja wa madereva walioshiriki tamasha hilo alisema ushiriki wa benki hiyo umewapa fursa ya kufahamu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kusimamia na kulinda shughuli zao za kila siku.
“Ni jambo zuri kuona taasisi za kifedha zikija karibu nasi na kutuletea huduma zinazozingatia mahitaji yetu. Kazi yetu ya kila siku inategemea vyombo vyetu vya usafiri na uwezo wetu wa kuendelea kufanya kazi ili kupata kipato.

“Kwa hiyo, kufahamu huduma za malipo na bima zinazoweza kutusaidia kulinda kazi zetu ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwetu,” alisema.
Kupitia ushiriki huo, Exim Bank inalenga kuongeza watumiaji wa Exim Lipa ChapChap, kuwafikia wateja wapya wa Tumaini Health Insurance na Motor Insurance, pamoja na kuongeza idadi ya akaunti za Exim Quick Account zinazofunguliwa.
Benki hiyo pia inalenga kujenga mahusiano ya muda mrefu na madereva, vikundi vyao na wadau wengine wa sekta ya usafiri kwa ajili ya fursa za ushirikiano wa baadaye.



