Akiba za wanachama PCCB Saccos zafikia bil 31.8/-

ARUSHA: CHAMA cha Akiba na Mikopo cha PCCB Saccos kimeendelea kuimarika kiuchumi, kikiongeza akiba za wanachama kutoka Sh bilioni 25.8 hadi Sh bilioni 31.8 ndani ya mwaka mmoja, hatua inayoongeza uwezo wa wanachama kupata huduma za kifedha kupitia chama hicho.
Ukuaji huo unaakisi mwitikio wa wanachama katika kuweka akiba na kuwekeza kupitia chama hicho kilicho chini ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Meneja wa PCCB Saccos, CPA Wilson Siwakwi, amesema idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 2,363 hadi 2,549 kati ya Oktoba 25 mwaka jana na Septemba 30 mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 7.9.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa chama hicho jijini Arusha, Siwakwi alisema hisa za wanachama pia zimeongezeka kutoka Sh bilioni 2.4 hadi Sh bilioni 2.8, huku uwekezaji katika Amana Maalumu ukipanda kutoka Sh milioni 666.8 hadi Sh bilioni 2.3.
Alisema mafanikio hayo yametokana na mikakati mbalimbali ya kuimarisha chama, ikiwemo uwekezaji wa pamoja wa Amana Maalumu ambapo kila mwanachama alitakiwa kuchangia Sh 100,000 kupitia mshahara wake ili kukamilisha uwekezaji wa Sh milioni moja.
Hata hivyo, alisema chama kinakabiliwa na changamoto ya mahitaji makubwa ya mikopo na huduma za chapchap ikilinganishwa na uwekezaji wa Amana Maalumu.

Katika hatua nyingine, alisema chama kinajiandaa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa sugu 47 walioshindwa kurejesha mikopo yao licha ya kukumbushwa mara kadhaa.



