Waajiri wasiotekeleza kima cha chini mshahara waonywa

ARUSHA; Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewaonya waajiri wa sekta binafsi ambao bado hawajatekeleza amri ya serikali kuhusu kima cha chini cha mshahara, akisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ili kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa stahiki zao.

Amesema utekelezaji wa amri hiyo umefikia takribani asilimia 90, lakini bado kuna waajiri ambao hawajazingatia viwango vilivyowekwa, hivyo Serikali inapanga kuwaita mwanzoni mwa Desemba waajiri kutoka sekta ambazo zimebainika kuwa na changamoto katika kutekeleza agizo hilo.

Sangu amewataka waajiri ambao bado hawajatekeleza amri hiyo kuanza mara moja kulipa mishahara kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kuhakikisha wanalipa malimbikizo yote kuanzia Januari mwaka huu, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wake, ili wafanyakazi wapate ujira wa haki kwa mujibu wa sheria na mikataba ya ajira.

Akizungumza jijini Arusha na waajiri kutoka sekta ya umma na binafsi pamoja na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Sangu pia amezitaka taasisi ambazo bado hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi kufanya hivyo haraka, akisema Serikali imepokea malalamiko kuhusu baadhi ya waajiri kutotambua umuhimu wa vyama vya wafanyakazi na mabaraza yao.

Awali Katibu Mkuu wa TUGHE, Rugemalila Rutatina, amelalamikia baadhi ya waajiri wanaokwamisha uundaji wa mabaraza ya wafanyakazi na wengine kuingilia uhuru wa watumishi kwa kuwachagulia vyama vya kujiunga navyo watumishi wapya wanaoajiriwa na kuongeza kuwa hali hiyo inakwamisha haki za wafanyakazi kushiriki katika maamuzi yanayowahusu na kuchagua vyama vitakavyowawakilisha

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button