Wafanyabiashara Moro wahamasishwa malipo kidigitali

MOROGORO:BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wafanyabiashara nchini kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali katika manunuzi na mauzo ya bidhaa zao, ikieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha katika uchumi na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na kubeba fedha taslimu.

Rai hiyo imetolewa na Ofisa wa BOT kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, Fredriki Mwakuu, wakati wa utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali na faida zake kwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Chifu Kingalu lililopo Manispaa ya Morogoro.

Mwakuu ni miongoni mwa watumishi wa BOT ambao ni wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya SHIMMUTA 2026  iliyoanza Novemba 6, mwaka huu na kutarajia kufikia tamati Novemba 21,2026 mkoani Morogoro.

Amesema BOT imebaini kuwa bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi na wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mifumo hiyo, hali inayochangia kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika huduma za malipo.

Amesema kutokana na hali hiyo, benki hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara ili kuongeza uelewa na matumizi sahihi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.

“Zipo changamoto nyingi ambazo Benki Kuu inazipata kutoka kwa watumiaji na jambo hilo limebainika kuwa linatokana na uelewa mdogo wa wananchi, wakiwemo wafanyabiashara,” amesema Mwakuu.

Ameongeza kuwa watumishi wa BOT wameamua kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao ya biashara ili kuwapatia elimu itakayowawezesha kunufaika na mifumo hiyo.

Mwakuu ametaja faida za malipo ya kidijitali kuwa ni pamoja na kuongeza usalama wa fedha, kuokoa muda, kurahisisha ulipaji wa kodi za serikali, kufanya malipo ya manunuzi ya bidhaa pamoja na kupokea fedha kutoka kwa wateja.

Amesema mifumo hiyo pia inasaidia wafanyabiashara kutunza kumbukumbu sahihi za miamala yao, jambo linaloweza kuwawezesha kupata huduma mbalimbali za kibenki, ikiwemo mikopo na kufungua akaunti.

“Mifumo hii ya malipo ya kidijitali inawasaidia kuweka vizuri kumbukumbu za miamala inayofanyika, ambazo zinawasaidia katika kupata huduma za kibenki, ikiwemo mikopo na kufungua akaunti,” amesema Mwakuu.

Amefafanua kuwa matumizi ya mifumo hiyo yanawasaidia wafanyabiashara kuepuka hatari za kubeba fedha taslimu, ikiwemo uwezekano wa kuibiwa au kudhurika, huku yakipunguza muda na gharama za kusafiri kwenda kufanya malipo katika maeneo yaliyo mbali.

Amesema mifumo hiyo hurahisisha uhamishaji wa fedha, malipo ya kibiashara na ulipaji wa huduma mbalimbali za serikali.

Amesema matumizi ya malipo ya kidijitali yanaweza kuongeza kasi ya biashara kwa kuwezesha wafanyabiashara kupokea malipo kwa wakati na hivyo kuchochea mzunguko wa fedha katika uchumi.

“Tunaamini kama mtu anatoa bidhaa yake na anapokea malipo kwa wakati, mauzo yataendelea kufanyika na mzunguko wa fedha utaongezeka. Hatimaye uchumi wa mfanyabiashara utakua na uchumi wa nchi utaimarika,” amesema Mwakuu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Chifu Kingalu, Manispaa ya Morogoro, Khalid Mkunyegele, ameipongeza BOT kwa kuwafikia wafanyabiashara hao na kutoa elimu kuhusu matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.

Mkunyegele amewataka wafanyabiashara wa soko hilo kuzingatia elimu waliyoipata kwa kutumia mifumo hiyo katika manunuzi na mauzo ili kupunguza hatari zinazotokana na kubeba fedha taslimu.

“Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa BOT kufika sokoni hapa kutoa elimu. Ninawaomba wafanyabiashara wa soko hili tufanye malipo na manunuzi kwa njia ya mifumo ya kidijitali, tuachane na kubeba fedha mkononi kwa kuwa huko ni kuhatarisha maisha yetu,” amesema

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Nafaka katika soko hilo, Evariste Moreka, aliiomba BOT kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kudhibiti changamoto za wizi wa fedha kupitia mitandao ya simu na akaunti za benki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button