Museveni aanza ziara Tanzania

RAIS wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ziara rasmi ya siku mbili kuanzia Agosti 5 hadi 6, 2026, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Rais Museveni na ujumbe wake wamepokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Mahmoud Thabit Kombo. Wengine waliompokea ni Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Museveni anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Samia, Ikulu jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yatajikita katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, biashara, uwekezaji, miundombinu na sekta nyingine za kimkakati kwa manufaa ya Tanzania na Uganda.
Hii ni ziara ya pili ya Rais Museveni nchini Tanzania katika mwaka 2026. Ziara yake ya kwanza ilifanyika Februari mwaka huu, ambapo yeye na Rais Samia walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili, pamoja na utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC).
Matarajio ya ziara hii ni kutoa msukumo mpya katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi hao, huku ikiendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Uganda kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.SOMA: Rais Museveni, Kikwete wakutana Uganda



