Siasa za Kijiografia Zinazoizunguka makubaliano ya afya kati ya Tanzania na Marekani

TANZANIA: Uamuzi wa Tanzania kuingia katika ushirikiano wa miaka mitano wa afya na Marekani unazidi kuwa zaidi ya makubaliano ya nchi mbili. Katika duru za kidiplomasia na afya ya umma, makubaliano hayo yanaonekana kama jaribio la awali la kuona kama nchi za Afrika zinaweza kujadiliana kuhusu ushirikiano mkubwa wa kimataifa unaoleta uwekezaji huku zikilinda vipaumbele vya kitaifa.
Makubaliano hayo yaliyotangazwa mwezi Julai yanaipa Marekani wajibu wa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.3 katika sekta ya afya ya Tanzania hadi mwaka 2030, huku Tanzania ikiahidi kuongeza matumizi yake ya ndani katika sekta hiyo.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha programu zinazolenga mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, kifua kikuu, malaria, afya ya mama na mtoto, ufuatiliaji wa magonjwa, mifumo ya maabara na miundombinu ya afya ya kidijitali.
Hata hivyo, umuhimu wa makubaliano hayo unaenda zaidi ya thamani yake ya kifedha.
Kwa miongo kadhaa, uhusiano kati ya Afrika na wafadhili wa kimataifa ulijengwa zaidi katika mfumo ambao mataifa tajiri yalitoa fedha, huku serikali za Afrika zikitekeleza programu ambazo mara nyingi ziliandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya wafadhili.
Mfumo huo sasa unaanza kubadilika.
Marekani imeendelea kuonyesha kuwa ushirikiano wake wa baadaye utaweka mkazo zaidi kwenye kuongeza fedha za ndani, kujenga uwezo wa taasisi na kuhakikisha mifumo ya afya inaweza kujiendesha kwa muda mrefu badala ya kutegemea misaada ya nje bila kikomo.
Makubaliano ya Tanzania na Marekani yanaonyesha mwelekeo huo mpya, ambapo uwekezaji wa nje unaambatana na matarajio kwamba serikali za kitaifa zitaendelea kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kugharamia na kusimamia mifumo yao ya afya.
Kwa Tanzania, makubaliano hayo yanatoa fursa ya kuboresha maeneo muhimu ya mfumo wa afya wakati ambapo nchi nyingi zinazoendelea bado zinakabiliwa na changamoto za kugharamia huduma za afya baada ya janga la COVID-19 na mabadiliko ya hali ya uchumi duniani.
Hata hivyo, ushirikiano huo pia umeibua mjadala kuhusu suala nyeti katika diplomasia ya kisasa ya afya uhuru wa kitaifa (sovereignty).
Tofauti na ushirikiano wa zamani uliolenga zaidi dawa na ujenzi wa hospitali, mikataba ya afya ya sasa inahusisha pia majukwaa ya afya ya kidijitali, mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, tafiti za vinasaba na kiasi kikubwa cha taarifa za afya.
Rasilimali hizo zimekuwa muhimu kimkakati kwa sababu zinaathiri tafiti za kisayansi, uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na ubunifu wa tiba za baadaye.
Ndiyo maana maswali kuhusu matumizi ya sampuli za kibaolojia na taarifa za afya yamevutia mjadala mkubwa karibu sawa na thamani ya fedha zilizotengwa kwenye makubaliano hayo.
Akijibu hofu za wananchi, Waziri wa Afya wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa, alisema kuwa nchi haikusaini makubaliano yoyote yanayoruhusu utoaji holela wa sampuli za kibaolojia kwa Marekani, akisisitiza kuwa sampuli hizo zitaendelea kuwa chini ya mamlaka ya Tanzania na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Pamoja na maelezo hayo, wataalamu wa masuala ya utawala wanasema uwazi bado ni jambo muhimu.
Ingawa maelezo ya serikali yamepunguza baadhi ya wasiwasi, wachambuzi wa sera wanaamini kuwa kuwekwa wazi kwa waraka kamili wa makubaliano hayo kungewezesha wataalamu wa sheria, watafiti na taasisi za kiraia kutathmini kwa uhuru namna masuala kama usimamizi wa taarifa, ushirikiano wa utafiti na haki za ubunifu yanavyoshughulikiwa.
Mjadala huu si wa Tanzania pekee.
Barani Afrika, serikali nyingi zinazidi kutathmini upya namna zinavyoshirikiana na washirika wa nje. Ushindani unaoongezeka wa kisiasa duniani umefanya sekta kama afya, miundombinu, teknolojia na nishati kuwa sehemu muhimu za diplomasia ya kimataifa.
China imepanua uwepo wake kupitia ujenzi wa hospitali, wataalamu wa afya na ushirikiano wa dawa. Umoja wa Ulaya umeongeza uwekezaji kupitia mpango wake wa Global Gateway, huku Marekani ikibadilisha namna inavyoshirikiana na Afrika kwa kulenga kujenga taasisi za ndani huku ikiendelea kudumisha uhusiano wa kimkakati wa muda mrefu.
Katika mazingira hayo, makubaliano ya Tanzania na Marekani yanaangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi wa kisiasa duniani.
Badala ya kuuliza kama Tanzania imekubali au imekataa msaada wa kigeni, wachambuzi sasa wanauliza swali tofauti:
Je, nchi za Afrika zinaweza kujadiliana kuhusu ushirikiano kwa masharti yanayoakisi vipaumbele vyao vya kitaifa huku zikivutia uwekezaji mkubwa wa kimataifa?
Jibu la swali hilo linaweza kuamua namna mikataba ya baadaye barani Afrika itakavyoundwa.
Wanaounga mkono ushirikiano huo wanasema kukataa msaada wa kimataifa hakutamaliza changamoto za kifedha wala kuimarisha huduma za afya.
Badala yake, wanasema kipaumbele kinapaswa kuwa kujadiliana kuhusu mikataba inayoongeza uwezo wa ndani, kuhamisha maarifa, kujenga wataalamu wa ndani na kuacha taasisi zikiwa imara baada ya ufadhili wa nje kumalizika.
Wakosoaji nao wanasisitiza kuwa uwekezaji wa kifedha pekee haupaswi kuchukua nafasi ya uwajibikaji wa umma.
Wanasema uwazi, usimamizi wa Bunge na ulinzi wa kisheria ni muhimu ili serikali ziweze kujenga imani ya wananchi katika makubaliano muhimu ya kimataifa.
Matokeo ya ushirikiano wa Tanzania na Marekani yanaweza hivyo kuathiri zaidi ya mfumo wa afya wa nchi hiyo pekee.
Iwapo mpango huo utafanikiwa kuboresha huduma za afya huku ukihifadhi udhibiti wa kitaifa juu ya rasilimali muhimu za afya, unaweza kuwa mfano wa ushirikiano wa baadaye kati ya serikali za Afrika na washirika wa kimataifa.
Lakini iwapo kutakuwa na mapungufu katika utekelezaji au masuala ya uwazi yataendelea kuleta mashaka, unaweza kuongeza taharuki kuhusu mikataba kama hiyo katika maeneo mengine ya Afrika.
Kwa ujumla, Tanzania imekuwa zaidi ya mpokeaji wa uwekezaji mkubwa wa afya. Imegeuka kuwa mfano wa kuangaliwa katika mabadiliko mapya ya diplomasia ya afya duniani ambapo mafanikio ya ushirikiano hayapimwi tena kwa ukubwa wa fedha pekee, bali kwa namna unavyoimarisha taasisi za kitaifa, kuheshimu mamlaka ya nchi na kutoa manufaa ya kudumu kwa wananchi.



