Tanzania kupunguza utegemezi dawa kutoka nje

MAREKANI: Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje na kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika.

Mchengerwa amesema hayo leo jijini New York, Marekani, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028, ambapo aliiwakilisha Tanzania katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo.

Kikao hicho, kilichoandaliwa na Serikali ya Sierra Leone, kinafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa 81 (UNGA 81), unaofanyika New York.

Katika kikao hicho, Mchengerwa amesema Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030, unaolenga kufikia malengo ya ‘Zero Tatu’, ikiwemo kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani usio na wataalamu, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga pamoja na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

“Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero Tatu,” amesema.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuhakikisha huduma za afya zinapatikana karibu na wananchi, huku ikiimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote na upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama na mtoto.

Mchengerwa amesema Serikali pia inaendelea kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha katika kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, ufadhili wa vituo vya kutolea huduma za afya, mifumo ya malipo ya kielektroniki, tozo maalum na huduma za utalii tiba.

Amesema Serikali inaendelea kuongeza mgao wa bajeti kwa huduma za afya ya msingi pamoja na huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga.

Akizungumzia umuhimu wa uzalishaji wa ndani, Mchengerwa amesema Afrika hutumia zaidi ya dola bilioni 28 za Marekani kila mwaka kununua dawa na bidhaa za afya, huku sehemu kubwa ya mahitaji hayo ikitoka nje ya bara.

Amesema hali hiyo inaweza kuziweka nchi katika hatari ya kukumbwa na changamoto za minyororo ya usambazaji pamoja na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania imeweka uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya, vifaa tiba na vifaa vya hospitali kuwa kipaumbele cha kitaifa, akisisitiza kuwa hatua hiyo si suala la uchumi pekee bali pia ni msingi wa kuimarisha usalama wa afya.

Amesema uzalishaji wa ndani utasaidia kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinaendelea kupata mahitaji muhimu hata pale kunapokuwa na changamoto katika minyororo ya usambazaji duniani.

Waziri huyo ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na washirika wa maendeleo kuunganisha nguvu katika uwekezaji wa sekta ya afya, uhamishaji wa teknolojia na sera za viwanda ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika.

Pia amesisitiza umuhimu wa kujenga minyororo ya thamani ya kikanda, kuimarisha mamlaka za udhibiti na kuunga mkono ubunifu unaozalishwa barani Afrika.

“Tanzania inaendelea kuhakikisha huduma muhimu za afya zinapatikana ndani ya umbali usiozidi kilomita tano kutoka kwa kila jamii, huku hospitali za rufaa zikitumika zaidi kwa wagonjwa wenye mahitaji ya huduma maalum,” amesema.

Mkutano wa UNGA 81 unawakutanisha wawakilishi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambapo viongozi hutumia jukwaa hilo kueleza misimamo na vipaumbele vyao kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo ni amani na usalama, vita na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, akili mnemba (AI), afya ya dunia, maendeleo na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Kaulimbiu ya UNGA 81 ni “Restoring Trust, Managing Transformation”, inayomaanisha “Kurejesha Imani, Kusimamia Mabadiliko.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button