Aga Khan, NHIF zakubaliana huduma za saratani

DAR ES SALAAM; Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa utoaji wa huduma za matibabu ya saratani kwa wanachama wa NHIF, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa katika hafla iliyofanyika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki, Dk Zeenat Sulaiman.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dk Isaka amesema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za NHIF za kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wanachama wake, hususan huduma za kibingwa zinazohitaji utaalamu na teknolojia maalumu.

Dk Isaka,amesema NHIF inaendelea kupanua wigo na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanachama wake, sambamba na kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma hizo kupitia mtandao wa watoa huduma wa mfuko.
“NHIF inaendelea kuboresha wigo na ubora wa huduma zinazopatikana kwa wanachama wake na kuongeza wigo wa vituo vinavyotoa huduma hizo.
“ Kusainiwa kwa makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya saratani kupitia mtandao wa watoa huduma wa mfuko,” amesema Dk Isaka.

Ameongeza kuwa makubaliano hayo yanaendeleza historia ya ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili na yamekuja wakati ambao Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa usawa na kwa wakati.
NHIF imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ushirikiano na watoa huduma mbalimbali wa afya nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wanachama wake, kuboresha ubora wa huduma na kuhakikisha matibabu yanatolewa kwa ufanisi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Dk Zeenat, amesema Hospitali ya Aga Khan inathamini ushirikiano huo na NHIF, akieleza kuwa makubaliano hayo yanaimarisha dhamira ya taasisi hizo mbili ya kushirikiana katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
“Ushirikiano huu unaonesha umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kushirikiana katika kuimarisha huduma za afya. Tutaendelea kutumia utaalamu, teknolojia na uzoefu wetu katika kutoa huduma za saratani kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu,” amesema.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wanachama wa NHIF watanufaika na huduma za matibabu ya saratani kwa wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam,Mwanza na kliniki 14 ikiwemo huduma za tiba kwa mionzi na tiba kwa kemikali.

Aidha, wanachama wa NHIF watapata fursa ya kuhudhuria kliniki za matibabu ya saratani katika hospitali hiyo na kupata huduma hizo kwa kuzingatia taratibu, masharti na miongozo ya mfuko.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza wigo wa vituo vinavyotoa huduma za matibabu ya saratani kwa wanachama wa NHIF, huku ikiwapa fursa ya kupata huduma za kibingwa kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu na kutumia teknolojia zinazohitajika katika matibabu ya ugonjwa huo.



