Huduma za jamii zaendelea kuimarika kijiji cha Makulu

DODOMA: Mkurugenzi wa Taasisi ya Igambilo, Gerald Ntyama, amesema taasisi hiyo imeendelea kuboresha maisha ya wananchi wa Kijiji cha Makulu, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, kupitia utekelezaji wa miradi ya maji safi, elimu na maendeleo ya jamii.
Ntyama amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, akieleza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kujenga kisima cha maji safi na salama kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, wananchi wa eneo hilo pamoja na Korea Hope Foundation, ambaye ndiye mfadhili mkuu wa mradi huo.

Amesema mchango wa taasisi hiyo ya ufadhili umekuwa wa muhimu katika kuhakikisha wananchi wa Makulu wanapata huduma ya maji safi na salama pamoja na fursa za maendeleo endelevu.
Ameipongeza Korea Hope Foundation kwa kujitolea kwake kufadhili miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, akisema ushirikiano huo umeleta matumaini mapya kwa jamii na kuwa mfano wa jinsi wadau wa maendeleo wanavyoweza kushirikiana na jamii kuleta mabadiliko chanya.

Ameeleza kuwa kabla ya mradi huo, wakazi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji kutoka katika vyanzo visivyo salama, hali iliyochangia kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji machafu.
Amesema upatikanaji wa maji kutoka kwenye kisima umeleta nafuu kubwa kwa wanawake na watoto waliokuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji, huku ukiwapa nafasi ya kushiriki katika shughuli nyingine za maendeleo.

Aidha, alisema mradi huo umechangia kupunguza hatari zinazoweza kuwakumba wanawake na watoto wanapokwenda kutafuta maji katika maeneo ya mbali.
Mbali na mradi wa maji, Taasisi ya Igambilo imeanzisha kilimo cha mboga mboga kwa kutumia umwagiliaji kutoka kwenye kisima hicho, ambapo wananchi wamepewa mafunzo ya kilimo bora na kuanza kuzalisha mazao kwa matumizi ya familia pamoja na kuuza sokoni ili kuongeza kipato.
Ntyama amesema taasisi hiyo pia imeanza kuwasaidia wananchi kulima alizeti na mtama kwa kutumia mifumo ya kisasa ya umwagiliaji (sprinkler), ambayo inasaidia kumwagilia eneo kubwa kwa muda mfupi hata wakati wa kiangazi.
Alibainisha kuwa hatua hiyo imeongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha usalama wa chakula pamoja na kipato cha wakulima.
Amewashukuru wananchi wa Makulu kwa ushirikiano wao tangu kuanza kwa mradi huo, akisema mafanikio yaliyopatikana yametokana na mshikamano kati ya wananchi, viongozi wa kijiji, Korea Hope Foundation na Taasisi ya Igambilo.
Alisisitiza kuwa Taasisi ya Igambilo itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza miradi mingine, hususan katika maeneo yenye changamoto ya ukame na upatikanaji wa maji.
Aidha, alisisitiza kuwa Taasisi ya Igambilo inaendelea kuthamini mchango wa Korea Hope Foundation, akieleza kuwa ufadhili wao umewezesha utekelezaji wa miradi yenye matokeo chanya kwa jamii na umechangia kuboresha maisha ya wananchi wa Makulu kwa kiwango kikubwa.



